DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU NI IPI?
Kila mtu huzaliwa katika mazingira au hali ambayo si chaguo lake mwenyewe.
Hupachikwa dini ya familia yake au mtazamo wa taifa lake toka mwanzoni mwa
kuwepo kwake katika dunia hii. Wakati anapofikia ujana wa (miaka 13 – 20),
kwa kawaida hulazimika kuamini kwamba imani ya jamii yake ndiyo imani
sahihi ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo. Ingawa wakati fulani baadhi ya
watu wanapokuwa wakubwa na wakaona imani nyingine huanza kuuliza na kuhoji
ukweli wa imani yao. Wale wanaotafuta ukweli mara kwa mara hufikia mahali
wakachanganyikiwa wanapogundua kwamba kila dini, dhehebu, au falsafa hudai
ndio njia pekee iliyo sahihi kwa mwanadamu, kwani makundi yote hayo
yanahamasisha watu kufanya matendo mema. Sasa ni ipi imani sahihi? Zote
haziwezi kuwa sahihi, kwani kila moja hudai kuwa nyingine zote si sahihi.
Sasa katika hali hiyo, yule anayetafuta ukweli vipi ataweza kuchagua njia
iliyosahihi?
Mwenyezi Mungu ametupa sote akili na uwezo wa kutuwezesha kufanya maamuzi
sahihi na ya maana. Nayo ni maamuzi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu.
Mustakabali wake unautegemea uamuzi huo, kufuatana na hilo, kila mmoja wetu
lazima achunguze ushahidi uliotolewa bila kupendelea ndipo achague kile
kinachoonekana kuwa ni sahihi mpaka pale ushahidi mwingine utakapotokea.
Kama ilivyo kwa kila dini au falsafa, Uislamu nao unadai kuwa huo ndio njia
ya pekee iliyo sahihi kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Katika hali hiyo ya
Uislamu kudai kuwa ni njia sahihi si tofauti na mifumo mingine. Kijitabu
hiki kinakusudia kukupa ushahidi juu ya ukweli wa dai hilo. Hata hivyo,
mara zote ni lazima izingatiwe kwamba, mtu anaweza kuipata njia ya kweli
kwa kuweka kando hisia na chuki, vitu ambavyo mara kwa mara hutupofua
tusiuone ukweli. Kisha, baada ya kufanya hivyo tu, ndipo tutakapoweza
kutumia akili zetu tulizopewa na Mwenyezi Mungu kufanya maamuzi ya kiakili
na yaliyo sahihi?
Kuna hoja mbali mbali ambazo zinaweza kutolewa ili kulipa nguvu dai la
Kiislamu kuwa ndio dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Zifuatazo ni hoja tatu
zilizo wazi sana. Ya kwanza inaegemea juu ya ukweli wa asili ya majina ya
dini na upana wa maana zake. Hoja ya pili inahusiana na mafundisho ya
kipekee na yasiyotatanisha yanayoonyesha uhusiano kati ya Mwenyezi Mungu,
mwanadamu na uumbaji. Hoja ya tatu inatokana na ukweli kwamba Uislamu ni
dini ya dunia nzima kwa watu wote na kwa nyakati zote. Hizi ndizo hoja tatu
za msingi ambazo kimantiki na kiakili zinalazimu ziwepo kwa dini yeyote ile
ili izingatiwe kuwa ni dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Kurasa zifuatazo
zitaufafanua ufahamu huo kikamilifu.
JINA LA DINI
Kitu cha kwanza kabisa ambacho mtu anapaswa kukijua na kukifahamu kwa kina
kuhusu Uislamu ni juu ya maana ya neno lenyewe “Uislamu.” Neno hilo ni la
asili ya Kiarabu lenye maana ya kutii au kusalimisha matakwa ya mtu kwa
Mwenyezi Mungu wa kweli wa pekee, ajulikanaye kwa Kiarabu kama “Allah”. Mtu
ambaye amesalimisha matakwa yake kwa Mwenyezi Mungu (Allah) huuitwa
“Mwislamu”. Dini ya Kiislamu haikupewa jina kutokana na jina mtu au watu,
wala halikuamuliwa na kizazi chochote cha wanadamu kama vile Ukristo ambao
ulipewa jina kutokana na “Yesu Kristo”, Ubudha unatokana na jina la Gautama
Buddha, Kunfushian, unatokana na Confucius, Umaksi ulipewa jina la Karl
Marx; Uyahudi unatokana na jina la kabila la Yuda na Ubaniani (Uhindu)
unatokana na jina la Hindu. Uislamu (kutii amri za Mwenyezi Mungu) ni dini
aliyopewa Adam, mtu wa kwanza na mtume wa kwanza wa Mwenyezi Mungu, na
Uislamu ndio dini ya mitume wote waliotumwa na Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.
Kwa kuongezea, jina la Uislamu lilichaguliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na
limetajwa wazi wazi katika kitabu cha mwisho cha Allah (Quran). Allah
alimfunulia mwanadamu katika kitabu cha mwisho alichomfunulia Mwanadamu.
Katika ufunuo wa mwisho, uitwao kwa Kiarabu Al-Quran Allah ameeleza
yafuatayo:-
“… Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na
Nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu…” [Quran 5:3]
“Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake…” [Quran
3:83]
Kwa hiyo, Uislamu haudai kuwa ni dini mpya iliyoletwa Arabuni na Mtume
Muhammad katika karne ya saba, lakini Uislamu ni mwendelezo wa sehemu ya
mwisho ya dini ya Allah, kama ilivyofunuliwa toka mwanzo kwa Adam na mitume
waliomfuatia.
Hadi kufikia hapa tutatoa maoni kwa ufupi kuhusu dini nyingine mbili
zinazodai kwamba ndizo njia sahihi. Hakuna sehemu yoyote katika Biblia
ambayo utakuta kwamba Mwenyezi Mungu amewafunulia watu wa Mtume Musa au
vizazi vyao kwamba dini yao inaitwa Uyahudi, au kwa wafuasi wa Kristo kuwa
dini yao inaitwa Ukristo. Kwa maneno mengine, majina “Uyahudi" na
"Ukristo” hayakutokana na asili ya Mwenyezi Mungu wala hayani idhini
yake. Jina Ukristo halikuwepo hadi muda mrefu baada ya kuondoka Yesu ndipo jina
hilo lilipotolewa kwa dini ya Yesu.
Sasa nini lililokuwa jina la kweli hasa, la dini ya Yesu, ambalo
linajipambanua na jina lake? (Majina yote mawili Yesu na Kristo yanatokana
na maneno ya Kiebrania, kupitia Kigiriki na Kilatini. Jesus ni Kingereza na
kwa Kilatini cha Kigiriki ni Iesous, ambalo kwa Kiebrania ni Yeshua au
Yehoshua' (Joshua). Neno la Kigiriki Christos ni tafsiri ya Kiebrania kwa
neno “Messiah”, jina la heshima linalomaanisha “Mpakwa mafuta.” Dini yake
inaakisi mafundisho yake, ambayo aliwaamrisha wafuasi wake kuyakubali kama
misingi ya kuwaongoza katika uhusiano wao na Mwenyezi Mungu. Katika
Uislamu, Yesu ni mtume aliyeletwa na Allah na jina lake la Kiarabu ni Issa.
Kama ilivyo kwa mitume ya kabla yake, yeye naye aliwalingania watu
wasalimishe matakwa yao kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu (jambo ambalo ndilo
linalosimamiwa na Uislamu). Kwa mfano katika Agano Jipya inasemekana kwamba
Yesu aliwafundisha wafuasi wake kusali kwa Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:-
“Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi
yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] (Luka 11:2/Mathayo 6:9).
Wazo hili lilisisitizwa sana na Yesu katika maelezo yake mengi
yaliyoandikwa katika Biblia. Kwa mfano, amefundisha kuwa, waliojisalimisha
kwa Mwenyezi Mungu, hao peke yao ndio watakaopata uzima wa milele.
(Peponi).
Yesu pia alifafanua kwamba yeye mwenyewe amejisalimisha kwa matakwa ya
Mwenyezi Mungu.
“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa
mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”
(Mathayo 7:21).
“Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na
hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali
mapenzi yake aliyenipeleka.” (Yohana 5:30).
Kuna maelezo mengi katika Biblia yanayoonesha kwamba Yesu aliweka wazi kwa
wafuasi wake kwamba yeye siye Mungu.
Kwa mfano, aliposema kuhusu saa ya mwisho alisema:
“Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio
mbinguni, wala Mwana, ila Baba. (Marko 13:-32).
Kwa hiyo, Yesu kama walivyokuwa Mitume waliopita kabla yake na yule
aliyekuja baada yake, alifundisha dini ya Kiislamu: kujisalimisha kwa
matakwa ya Mwenyezi Mungu mmoja aliye wa kweli.
MWENYEZI MUNGU NA UUMBAJI
Kwa vile jambo la mtu kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu
linamaanisha kiini cha kuabudu, ujumbe wa msingi wa dini ya Mwenyezi Mungu,
Uislamu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Vilevile Uislamu unawataka
watu waachane na kuabudu binadamu, eneo au kitu zaidi ya Mwenyezi Mungu.
Kwa vile vitu vyote ukimtoa Mwenyezi Mungu muumbaji wa vitu vyote, ni
uumbaji wa Mwenyezi Mungu; inawezekana kusemwa kwamba Uislamu kimsingi
unamlingania mtu aache kuabudu viumbe na kumwita amwabudu muumbaji wake
pekee. Yeye ndiye pekee anayestahiki kuabudiwa na watu, kwa sababu ni kwa
matakwa yake yeye tu ndipo maombi yote hujibiwa.
Kutokana na hilo, endapo mwanadamu atauomba mti na maombi yake kujibiwa,
basi akumbuke kwamba si mti uliojibu maombi yake bali ni Mwenyezi Mungu,
ndiye aliyeruhusu maombi hayo yawe kama alivyoomba. Mtu anaweza kusema,
“jambo hilo lipowazi”. Hata hivyo, kwa wale wanaoabudu miti, inawezekana
isiwe hivyo. Vivyo hivyo, wale wanaomwabudu Yesu, Budha, au Krishna au
mtakatifu Kristofa, au mtakatifu Jude au hata Muhammad, maombi yao
hayajibiwi na hao, bali yanajibiwa na Mwenyezi Mungu. Yesu hakuwaambia
wafuasi wake wamwabudu yeye bali aliwaambia wamwabudu Mwenyezi Mungu, kama
inavyoeleza Quran:
"Na (kumbukeni) Mwenyezi Mungu atakaposema: "Ewe Isa bin Maryamu!
Je, wewe uliwaambia watu: 'Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa waungu badala
ya Mwenyezi Mungu'?" Aseme (Nabii Isa): "Wewe umetakasika na kuwa
na mshirika. Hainijuzii mimi kusema ambayo si haki yangu (kuyasema, kwa
kuwa ni ya uwongo). (Quran 5:116)
Yesu hajajiabudu yeye mwenyewe alipokuwa anaabudu, lakini alimwabudu
Mwenyezi Mungu. Yesu amenukuliwa ndani ya Biblia akisema,
“…Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” (Luka
4:8).
Kanuni hii ya msingi ipo katika sura ya kwanza katika Quran ijulikanayo
kama Suratul-Fatiha, aya ya nne
“Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na Wewe tu ndiye tunayekuomba msaada.” (Quran
1:5)
Na katika sehemu nyingine ndani ya Kitabu cha ufunuo wa mwisho, ambacho ni
Quran, pia Mwenyezi Mungu amesema:
“Na Mola wenu Anasema: “Niombeni Nitakujibuni.” (Quran 4:60)
Ni muhimu mno kusisitiza kwamba msingi wa ujumbe wa Uislamu (umetaja
kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake) pia umetangaza kwamba Mwenyezi Mungu na
viumbe vyake ni tofauti kabisa. Mwenyezi Mungu hayuko sawa na viumbe vyake
wala si sehemu ya viumbe vyake, na wala viumbe vyake si sawa Naye na wala
si sehemu ya Uungu.
Hili lawezekana kuonekana ni jambo lililowazi, lakini kitendo cha mwanadamu
kuabudu viumbe, badala ya Muumba kwa kiasi kikubwa Kinatokana na ujinga au kupuuza,
ufahamu huu. Ni imani ya baadhi ya watu kwamba kuwepo kwa Mwenyezi
Mungu kupo kila mahala katika viumbe vyake au kuwepo kwa uungu wake kupo au
kulikuwepo katika baadhi ya sehemu za viumbe vyake, jambo lilowahalalishia
waabudu viumbe vya Mwenyezi Mungu na kusema kuwa wanamwabudu Mungu. Hata
hivyo, ujumbe wa Uislamu kama ulivyoletwa na Mitume ya Mwenyezi Mungu, ni
kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuacha kuabudu viumbe vyake kwa moja
kwa moja au kwa kutumia njia yoyote ile.
Katika Quran Mwenyezi Mungu amesema wazi wazi:
“Na bila shaka Tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba: “Muabuduni
Mwenyezi Mungu na mwepukeni (Iblisi) muovu.” (Quran 16:36)
Wakati wale wanaoabudia masanamu wanapoulizwa; kwa nini wanaabudu masanamu
yaliyotengeneza na Wanadamu? Jibu la siku zote ni kuwa; kwa hakika wao
hawaiabudu ile picha ya jiwe bali wanaabudia Mwenyezi Mungu aliyopo katika
masanamu hayo. Wanadai kwamba masanamu hayo ni sehemu za kumuelekea
Mwenyezi Mungu tu na si Mwenyezi Mungu mwenyewe! Mtu aliyekubali wazo la
kuwa Mwenyezi Mungu kwa namna yoyote ile yupo ndani ya viumbe vyake
atalazimika kukubali hoja hii ya kuabudu masanamu. Wakati, mtu aliyeufahamu
vizuri msingi wa ujumbe wa Uislamu na utekelezwaji wake kamwe hawezi
kukubali kuabudia masanamu hata kama kutajengewa hoja za kimantiki.
Wale waliodai ungu tangu zamani mara kwa mara wameelekeza madai yao katika
imani potofu ya kwamba Mwenyezi Mungu yu katika mwanadamu. Tukienda hatua
moja mbele, wanadai kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja nao kuliko alivyo kwetu
sisi tuliobakia, kwa hiyo, wanadamu wanapaswa kunyenyekea kwao na kuwaabudu
wao kama vile Mwenyezi Mungu aliye katika mwanadamu au Mwenyezi Mungu
aliejiingiza kwa wanadamu. Vilevile wale wanaotangaza uungu wa watu wengine
baada ya kufa kwao wamepata ardhi yenye rutba miongoni mwa wale wanaoamini
imani potofu ya kuwa Mwenyezi Mungu yupo ndani ya mwanadamu.
Hadi sasa hivi, lazima iwe wazi kabisa kwamba mtu aliyeelewa msingi wa
ujumbe wa Uislamu na vidokezo vyake kamwe hawezi kukubali kumwabudu mwadamu
mwenzake katika hali yoyote ile. Dini ya Mwenyezi Mungu, kwa asili, ni wito
uliowazi wa kumwabudu Muumba na kukataa kuabudu viumbe kwa namna yoyote
ile. Na hii ndio maana ya wito wa Uislamu.
"Laa Ilaha Ill Allah" (Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah).
Kutamka kwa dhati ibara hii na kumkubali Mtume, moja kwa moja kunampelekea
mtu kuwa katika Uislamu, na imani ya dhati kwa tamko hilo
humuhakikishia mtu kuingia Peponi. Kwa hiyo, Mtume wa mwisho wa Uislamu
(S.A.W) amenukuliwa akisema kuwa, “Yeyote asemaye: Hakuna Mungu wa haki
ispokuwa Allah, na akafa akiwa na imani hiyo ataingia Peponi.”
Imani juu ya tamko hili la kiitikadi inamtaka mtu kusalimisha matakwa yake
kwa Mwenyezi Mungu kwa namna zilizofundishwa na Mitume ya Mwenyezi Mungu.
Vilevile tamko hilo linamtaka muumini aache kuabudu miungu ya uongo.
UJUMBE WA DINI ZA UWONGO
Kuna madhehebu, makundi ya kidini, dini, falsafa, na harakati nyingi
duniani, yote hayo yanadai kuwa ndio njia sahihi au ndio njia ya pekee ya
Mwenyezi Mungu. Sasa vipi mtu ataweza kugundua ni kundi lipi lililosahihi
au kama yote ni sahihi? Njia moja ya kupata jibu la swali hilo ni kuondoa
tofauti za kijuu juu, katika mafundisho ya wadai mbali mbali ili kuufikia
ukweli, na kutambua kitu kikuu kinachoabudiwa na kitu hicho ndicho hasa
wanachokilingania, moja kwa moja au sio moja kwa moja. Dini za uongo zote,
kikawaida, zina hoja moja maarufu iliyo ya msingi juu ya Mwenyezi Mungu,
aidha wanadai wanaume wote ni miungu, au wanaume fulani tu ndiyo miungu au
maumbile (nature) ndiyo Mwenyezi Mungu au Mwenyezi Mungu ni kitu kilichopo
tu katika dhana za watu.
Kwa hiyo, kuna uwezekano wa kusema kwamba, msingi wa ujumbe wa dini za
uongo ni kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuabudiwa kwa mfumo wa umbaji wake.
Dini za uongo huwaita watu waabudu viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa kuviita
viumbe hivyo au sehemu ya viumbe hivyo ni Mwenyezi Mungu. Kwa mfano, Nabii
Issa (Yesu) aliwaita, wafuasi wake wamwabudu Mwenyezi Mungu, lakini wale
wanaodai kuwa wao ni wafuasi wa Yesu leo hii wanawalingania watu wamwabudu
Issa (Yesu), wakidai kwamba yeye ni Mwenyezi Mungu.
Budha alikuwa mrekebishaji ambaye alianzisha kanuni mbali mbali za
kibinadamu katika dini ya Kihindu. Hakudai kuwa yeye ndiye Mungu mwenyewe,
wala hakupendekeza kwa wafuasi wake kwamba yeye awe wa kuabudiwa. Leo hii,
Mabudha wengi mno walio nje ya India wanamfanya yeye (Budha) kuwa ni
Mwenyezi Mungu na wanasujudia masanamu yaliyotengenezwa kwa sura yake.
Kwa kutumia msingi wa kutambua kitu kinachoabudiwa, tunaweza kuzigundua kwa
urahisi dini za uongo na asili ya vyanzo vyake.
Kama Mwenyezi Mungu alivyosema katika Quran:
“Hamuabudu badala yake (Mwenyezi Mungu ila majina (matupu) mliyoyapanga
nyinyi wenyewe na baba zenu (mkayaita hayo masanamu). Mwenyezi Mungu
hakuteremsha dalili kwa hayo. Haikuwa hukumu ila hii ya Mwenyezi Mungu tu;
Ameamrisha msimuabudu yoyote ispokuwa Yeye tu. Hiyo ni Dini madhubuti,
lakini watu wengi hawajui”. (Quran 12:40)
Watu wanaweza kutoa hoja kwamba dini zote zinafundisha mema, kwa hiyo, kuna
haja gani ya kujali kuifuata dini mojawapo? Jibu ni kwamba dini za uwongo
zote zinafundisha dhambi kubwa sana ya kuabudu viumbe. Kuabudu viumbe ni
dhambi kubwa kabisa awezayo kuifanya mwanadamu kwa sababu tendo hilo
linapingana na lengo la kuumbwa kwake.
Mwanadamu ameumbwa ili kumwabudu Mwenyezi Mungu tu kama Allah alivyosema
katika Quran:
“Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu”. (Quran 51:56)
Matokeo yake, kuabudu viumbe; jambo ambalo ni asili ya kuabudu masanamu ni
dhambi pekee isiyosameheka. Mtu atakayekufa katika hali hiyo ya kuabudu
masanamu, ameshaangamiza majaaliwa yake ya ahera. Hii si rai ya mtu, bali
ni ufunuo wa kweli ulioelezwa na Mwenyezi Mungu katika ufunuo wake wa
mwisho kwa wanadamu:
“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa; na Husamehe yasiyokuwa haya
kwa amtakaye. (4:48 na 116)
DINI YA MWENYEZI MUNGU NI YA ULIMWENGU MZIMA
Kwa vile matokeo ya kufuata dini ya uwongo ni hatari sana, dini ya kweli ya
Mwenyezi Mungu ni lazima ifahamike dunia nzima, iwe imepatikana dunia nzima
wakati uliopita na lazima idumu milele na iwe inafahamika milele na
ipatikane dunia zima. Kwa maneno mengine, dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu
haiwezi kuwa na mipaka kwa watu fulani tu, eneo, au kipindi fulani tu. Wala
si jambo la kimantiki kwamba dini kama hiyo iamuru mazingira yasiyo na
maana yoyote katika uhusiano kati ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu kama vile,
kubatiza, au imani kwamba mwanadamu ni mwokozi, au ni mpatanishi. Katika
kanuni kuu ya Uislamu na ambayo maana yake ni (kusalimisha matakwa ya mtu
kwa Mwenyezi Mungu) ndipo inapopatikana mizizi ya Uislamu kuwa wa dunia
nzima. Wakati wowote mwanadamu anapotambua kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na
ametofautiana na viumbe vyake, na mtu huyo akajisalimisha kwa Mwenyezi
Mungu, Mtu huyo anakuwa Mwislamu kimwili na kiroho na anastahiki Pepo.
Kwa hiyo, mtu yoyote katika muda wowote hata yule aishiye maeneo ya mbali
anaweza kuwa Mwislamu, mfuasi wa dini ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, kwa
kukataa moja kwa moja kuabudu viumbe na kuamua kumgeukia Mwenyezi Mungu
peke yake.
Ni lazima ikumbukwe, hata hivyo, ili kujisalimisha kwa matakwa ya Mwenyezi
Mungu kikweli kweli, mtu ni lazima achague baina ya haki na batili. Kwa
hakika, binadamu amejaaliwa uwezo na Mwenyezi Mungu sio tu wa kutofautisha
kati ya wema na uwovu bali vilevile kuchagua kati ya vitu viwili hivyo.
Huu uwezo wa kupewa na Mwenyezi Mungu unabeba majukumu muhimu sana, nayo ni
kuwa, mwanadamu atajibu kwa Mwenyezi Mungu juu ya chaguo alilolichagua.
Kinachofuata mwanadamu anapaswa ajaribu kwa kutumia uwezo wake wote afanye
mema na aache maovu.
Ufahamu huu umeelezwa katika ufunuo wa mwisho kama ifuatavyo:
“Katika walioamini (Mitume ya zamani huko) na Mayahudi na Wakristo na
Wasabai; yoyote (miongoni mwao) atakayemwamini Mwenyezi Mungu (sasa kama
anavyosema Nabii Muhammad) na akaamini Siku ya Mwisho na akafanya vitendo
vizuri, basi watapata thawabu zao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu
yao, wala hawatahuzunika. (Quran 2:62)
Ikiwa kwa sababu yoyote ile, wanadamu watashindwa kuukubali ujumbe wa
mwisho baada ya kuelezwa bayana, watakuwa katika hatari kubwa mno. Mtume wa
mwisho amesema:
"Yoyote miongoni mwa Wakristo na Wayahudi atakayesikia habari zangu na
akaendelea na imani ya kukakanusha kile nilichokuja nacho na akafa katika
hali hiyo atakuwa ni miongoni mwa wakazi wa Motoni."
(Sahih Muslim [English Translation], Vol.1 p.91 N0, 284)
KUMTAMBUA MWENYEZI MUNGU.
Swali linalojitokeza hapa ni: vipi itarajiwe kuwa watu wote watamwamini
Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli, ukizingatia watu hao wana asili za jamii na
tamaduni tofauti tofauti? Ili watu wawajibike kwa kumwabudu Mwenyezi Mungu
mmoja wa kweli, wanahitaji wapate elimu ya kumtambua Mwenyezi Mungu. Ufunuo
wa mwisho unafundisha kwamba wanadamu wote wana athari ya kumtambua Mungu
mmoja wa kweli athari ambayo iliwekwa katika nafsi zao ikiwa ni kama sehemu
ya asili yao waliyoumbiwa nayo.
Katika sura ya saba ya Quran (Al-Aaraf, aya ya 172 – 173), Mwenyezi Mungu
ameeleza kwamba wakati alipomuumba Adam alijaalia kizazi cha Adam kuwepo
ulimwenguni na Mwenyezi Mungu akuchukua ahadi toka kwao na kuwaambia: “Je,
Mimi siye Mola wenu?" Wakasema: “Ndiye; tunashuhudia (kuwa Wewe ndiye
Mola wetu)."
Kisha Allah akaeleza sabababu za kuwalazimisha wanadamu wote wakiri kwamba
yeye ndiyo muumba wao na ndiye Mwenyezi Mungu wa kweli wa pekee
anayestahiki kuabudiwa. Amesema:
“Msije mkasema Siku ya Kiyama kuwa sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo
(hatuyajui). (Quran 7:172)
Hii inamaanisha kwamba, hatuwezi kudai katika siku hiyo kwamba tulikuwa
hatujui kuwa Allah ndiye Mungu wetu na kwamba hakuna mtu aliyetwambia
kwamba tulipaswa kumwabudu Allah peke yake. Allah akaendelea kuelezea kuwa:
“Au mkasema, Baba zetu ndio walioshirikisha zamani, nasi tulikuwa kizazi
nyuma yao, basi Utatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya waovu?”
(Hamuwezi kusema haya kwani nyote Tumekufahamisheni, nyinyi na wao). (Quran
7:173).
Kwa hiyo, kila mtoto huzaliwa na imani ya kumtambua Mwenyezi Mungu na
mwelekeo wa kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee. Imani hii ya kuzaliwa nayo na
mwelekeo huo huitwa kwa Kiarabu “Fitrah”.
Mtume Muhammad (S.A.W) ameeleza kwamba Allah amesema,
“Niliwaumba waja wangu katika dini sahihi, lakini shetani aliwapoteza.”
Vilevile Mtume amesema, “Kila mtoto huzaliwa katika Fitrah. Kisha wazazi
wake wanamfanya aidha awe Myahudi, Mkristo au Mmajusi (waabudio moto).’’
Ikiwa mtoto ataachwa peke yake, atamwabudu Mwenyezi Mungu kwa namna yake
mwenyewe, lakini watoto wote huathiriwa na mazingira. Kwa hiyo, ni kama
vile mtoto anatii sheria za kimaumbile, ambazo Allah ameziamrisha
kimaumbile, katika hali hiyo hiyo nafsi yake pia inatii maumbile ya kuwa
Allah ni Mola na Muumba wake. Lakini, ikiwa wazazi wake watajaribu kumfanya
afuate njia tofauti, mtoto anakuwa hana nguvu za kutosha, hasa hasa katika
hatua zake za mwanzo za maisha yake, za kuzuia na kupinga matakwa ya wazazi
wake.
Katka hali kama hizo, dini ambayo mtoto anaifuata, ni tamaduni na malezi,
na Mwenyezi Mungu hamuhesabu wala hamuadhibu kwa dini hiyo mpaka
atakapofikia umri fulani maishani mwake. (baleghe).
DALILI ZA MWENYEZI MUNGU.
Katika hatua zote za maisha ya wanadamu, kutoka utoto hadi kufikia
kufariki, dalili za Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli zinaonyeshwa kwao katika
pande zote za dunia na katika nafsi zao mpaka inapowabainikia kwamba kuna
Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli (Allah). Mwenyezi Mungu amesema
katika Quran:
“Tutawaonyesha (ukweli wa) Maneno Yetu haya katika nchi za mbali na katika
nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli…” (Quran: 41:53)
Ufuatao ni mfano wa ufunuo wa Mwenyezi Mungu kwa dalili ya kosa la mtu
mmoja la kuabudu sanamu. Katika maeneo ya kusini mashariki mwa msitu wa
Amazoni huko Brazili, Amerika ya Kusini watu wa kabila la wasiostaarabika
walijenga kibanda kipya ili kuhifadhi sanamu la mtu liitwalo Skwatch,
likiwa ni Mungu mkuu wa viumbe vyote.
Siku iliyofuatia kijana mmoja aliingia kibandani kutoa heshima kwa Mungu
huyo, na alipokuwa ameinama (kukisujudia) kile alichofunzwa kuwa ndicho
Muumba na Mpaji wake, ghafla mbwa mkondefu mwenye viroboto na mafunza
aliingia pole pole mule kibandani. Yule kijana aliinua kichwa chake kwa
kitambo kidogo akamtazama yule mbwa, akiinua mguu wake wa nyuma na
kulikojolea lile sanamu.
Yule kijana alimfukuza yule mbwa nje ya kile kibanda kikatili, lakini mara
tu ghadhabu zake zilipoisha alitambua kwamba lile sanamu kamwe haliwezi kuwa
Mola wa Ulimwengu wote. Mwenyezi Mungu, lazima atakuwa yupo sehemu
nyingine, alihitimisha. Ni jambo la kushangaza kama linavyoweza kuonekana,
mbwa kulikojolea lile sanamu ilikuwa ni alama kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa
kijana huyo. Alama hii imebeba ujumbe mtakatifu kwa kuwa kile alichokuwa
akikiabudu kilikuwa cha uwongo. Huo ni ukombozi kutoka utumwa wa kufuata
mafundisho ya utamaduni wa kuabudu mungu wa uongo. Matokeo yake, mtu huyu
amehiyarishwa: aidha amtafute Mwenyezi Mungu wa kweli au aendelee katika
njia yake ya makosa.
Allah (S.W) anataja utafutaji wa kumtafuta Mwenyezi Mungu unaomuhusu Mtume
Ibrahimu kuwa ni mfano wa jinsi ya wale wote wanaofuata dalili zake
wataongozwa katika njia sahihi.
“Na namna hivi Tulimwonyesha Ibrahimu ufalme wa mbingu na ardhi (kuwa ni wa
Mungu), na ili awe miongoni mwa wenye yakini. Na usiku ulipomwingilia
(Ibrahimu na hali kakaa na makafiri), akaona nyota, alinena (makusudi
kutaka kuwavuta watumie fikra zao): “(Nyota) hii ni Mola wangu.” Ilipotua
(ikapotea), alisema (kuwaambia wale makafiri kama kwamba yu pamoja nao
katika ibada ile): “Sipendi waola wanaopotea (hawawepo ila wakati makhsusi
tu).” Na (usiku wa pili) alipouona mwezi unachomoza alisema (kuwaambia wale
marafiki zake wa kikafiri): “Huu (mwezi) ndio Mola wangu.” Ulipotua
alisema: “Asiponiongoza Mola wangu, bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu
wapotofu. (Na mola huyu hawezi kuniongoza kwani anakuwa hayupo wakati
mwengine).” Na (siku ya tatu) alipoliona jua linachomoza alisema
(kuwaambia): “Hili (jua) ndilo Mola wangu. Huyu (mola) mkubwa kabisa,”
lilipotua alisema: “Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo
mnayoyashirikisha (na Mungu) “Mimi nimeuelekeza uso wangu kwa Yule
aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimewacha dini za upotevu. Mimi
(ni Mwislamu) wala si miongoni mwa washirikina.” (Quran 6:75-79)
Kama tulivyosema hapo mwanzoni, Mitume wametumwa kwa kila taifa na kila
kabila ili kuiwezesha imani ya kimaumbile ya mwanadamu juu ya Mwenyezi
Mungu na ule mwelekeo wa kumwabudu Yeye, pia kuutia nguvu ukweli
mtatakatifu kwa dalili na alama za kila siku zinazooneshwa na Mwenyezi
Mungu. Ingawa mafundisho mengi ya Mitume hao yamebadilishwa, baadhi ya
sehemu zinazofunua ujumbe wa zimebakia bila kuvurugwa na zinahudumia katika
kuwaongoza watu katika kuchagua kati ya haki na batili.
Athari za ujumbe uliofunuliwa na Mwenyezi Mungu kwa muda mrefu zinaweza
kuonekana katika "Amri Kumi" za Torati ya Wayahudi ambazo baadaye
ziligeuzwa na kuwa katika mafundisho ya Kikristo, vilevile, kuwepo kwa
sheri dhidi ya uuaji, wizi na uzinzi katika jamii nyingi kote kote katika
zama za kale na za sasa za ulimwengu.
Matokeo ya alama za Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wa zama zote zikiwa na
ufunuo wake kupitia Mitume yake, wanadamu wote wamepewa nafasi ya kumtambua
mungu wa kweli wa pekee.
Matokeo yake, kila nafsi itahesabiwa kwa imani yake juu ya Mwenyezi Mungu
na kwa kukubali kwake dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu, iitwayo Uislamu,
ambayo inamaanisha utiifu mkamilifu kwa matakwa ya Allah.
HITIMISHO
Maelezo yaliyotangulia yamefafanua kwamba jina la dini ya Kiislamu
linaeleza wazo kuu na la msingi la Uislamu, ni kujisalimisha kwa Mwenyezi
Mungu, na kwamba jina "Uislamu" halikuchaguliwa na mwanadamu,
bali lilichaguliwa na Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa vitabu vitakatifu vya
Uislamu. Vilevile imeoneshwa kwamba ni Uislamu pekee unaofundisha kwamba
Mwenyezi Mungu ni mmoja na Sifa zake na unaamrisha kumwabudu Mwenyezi Mungu
tu bila ya mshirika. Mwisho, kutokana na utakatifu wa mwelekeo ulioingizwa
pole pole kwa mwanadamu ili amwabudu Mwenyezi Mungu na dalili zilizooneshwa
na Mwenyezi Mungu kwa miaka mingi kwa kila mtu, Uislamu unaweza kufikiwa na
watu wote kwa nyakati zote.
Kwa ufupi, maana ya neno Uislamu (kujisalimisha kwa Allah), Uislamu
kikamilifu unakiri upweke wa Mwenyezi Mungu na ufikiwaji wa Uislamu kwa
watu wote katika nyakati zote kukinaisha watu kuunga mkono dai la Uislamu
la kwamba toka mwanzoni mwa Ulimwengu katika lugha zote imeelezwa kwamba,
Uislamu pekee ndio uliokuwa na utakaoendelea kuwa dini pekee ya kweli ya
Mwenyezi Mungu.
Tunahitimisha kwa kumuomba Allah, Mtukufu, atuweke katika njia iliyosahihi
ambayo ametuongoza kwayo, na atupatie baraka na rehema zake, kwani yeye ni
Mwingi wa msamaha. Shukrani ziende kwa Allah, Mola wa ulimwengu wote, na
rehema na amani ziende kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na kwa Mitume ya
Allah yote na kwa wafuasi wao waliowema.
|
0 comments:
Post a Comment