JOIN US ANGAZA.................................................JOIN US ANGAZA......................WELLCOM
Nav view search
Navigation
"Dini
ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake,
kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu
UMUHIMU WA SWALA NA NAFASI YAKE KATIKA UISLAMU
A: HUKUMU YA SWALA KWA MUJIBU WA QUR-ANI NA SUNNAH
Ewe
ndugu yangu mpenzi; hebu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tuzianze
nasaha zetu kwa kumuomba Mola wetu Mtukufu atuwafikshe na kutuongoza
katika kuijua haki, kuikubali na ksha kuifuata-Aamiyn Baada ya dua hiyo,
hebu sasa tutazame kwa pamoja natujiulize nini hukumu ya ibada ya swala
ndipo tutafahamu ni ipi nafasi na hukumu ya mtu asiye swali .
Ndugu yangu mpenzi, elewa na ufahamu kwamba swali katika sheria ni FARDH yaani WAJIBU.
Haya ni kwa mujibu wa aya chungu mzima za Qur-ani Tukufu. Hebu tusitafakari kwa pamoja aya hizi zifuatazo
"…BASI SIMAMISHENI SWALA, KWANI HAKIKA SWALA. IMEKUWA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA WAKATI MAALUM" [4:103]
Ukizingatia
aya hii utakuta inaeleza kwa ufumbulizo na uwazi kabisa kwamba swali ni
FARDHI, tenasi fardhi tu bali ni fardhi iliyowekewa wakati maalum na
Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake waumini kauli ya Mola karim
Aliposema:
"… HAKIKA SWALAKWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA WAKATI MAALUM "
ni ishara na dalili bayana kwamba swala ndio kielelezo kikubwa cha
Imani ya mja. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa hana Imani, mtu
asiyeswali.
Ikiwa mtu hana Imani , vipi unamtazamia kuwa na dini? Hii ndio maana Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie akasema:
Mkimuona
mtu aizoya Msikiti basi mshudieni kuwa yuna Imani kauli hii ya Bwana
Mtume inazidi kutuonyesha ukweli usio pingika kwamba swala ndio nembo na
kielelezo kikubwa cha Imani ya mja. Hebu tuitafakari na aya hii:-
"HIFADHINI (angalieni sana) SWALA (zote kuziswali) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI "[2:238]
Tukilizingatia
neno la mwanzo lilotumika katika aya (HIFADHINI) tukaliweka katika
sarufi ya kiarabu (Arabic Grammar), tutaambiwa na watu wa fani ya lugha
kuwa neno hili ni tendo la amri.
Kwa
hivyo basi neno hili (HIFADHINI) inbamaanisha kuwa suala la kuhifadhi
swala ni amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa waja wake na wala sio
ombi.
Sasa
kama tunakubaliana na ukweli huu ulio dhahiri kuwa swala ni amri ya
Mola amuamrisha mja wake, je! Huoni kwamba kuacha swala ni kupinga na
kuivunja amri ya Muumba wako?
Avunjaye
na kupinga amri ya Bwana wake hufanywaje na Bwana wake, hasa
ukizingatia kwamba siku zote amri hutoka kwa Mkubwa aliye kuja juu kwa
mdogo aliye chini kama ambavyo ombi hutoka kwa aliye chini kuja kwa
aliye juu.
Hebu
jaribu kuwa mkweli, mwanao au mkeo akivunja amri yako, unakuwaje na
unchukua hatua gani? Ukiukir ukweli huu ndipo utaiona nafasi yako mbele
ya Mola wako wewe usiyetaka kumsujudia Mola wako.
Naam,
tumetangulia kusema huko nyuma kwamba swala ni FARDHI /WAJIBU, hebu
sasa tulitazame neno WAJIBU limeaanishwa vipi na sheria ili uione nafasi
yako wewe usiyeswali.
Wataalamu
wa fani ya fiq-hi wamelianisha neno wajibukwa kusema (WAJIBU/FARDHI ni
lile jambo ambalo Allah ameliwajibisha juu yetu, hulipwa mtu aliye
baleghe (mtu mzima),mwenye akili timamu kwa kulitenda/kulitekeleza (hilo
la wajibu)na huaadhibiwa kwa kuwacha kulitenda, kama vile swala, funga
na kuwatii wazazi).
Hili ndilo ainisho (definition) sahali la WAJIBU, hebu sasa lichukuwe aanisho hili uliambatishe na swala, unafahamu nini?
Ikiwa
wewe ni mkweli, uliokulazimu kwa amri ya Mola Muumba wako na kwamba
ukiswali utakuwa umeikubali na kuipokea kuitekeleza amri ya Mola wako
kwa maslahi na faida ya nafsi yako, hivyo utalipwa thawabu ambaazo ndizo
"Dollar" za kuinunulia akhera.
Kinyume
chake ni kwamba kama hukuswali utakuwa umeipuzana na kuivunja amri ya
Molawako kwa maangamivu na khasara ya nafsi yako mwenyewe, kwa hivyo
utaaadhibiwa kwanza hapa hapa duniani, kaburini na kesho akhera kama
lilivyothibiti hilo katika hadithi ya Mtume –Rehema na Amani zimshukie.
Tusome kwa mazingatio:
"… NA BILA SHAKA ADHABU YA AKHERA NI KALI ZAIDI NA IENDELEAYO SANA"[20:127]
"ANAYEFANYA
MEMA ANAJIFANYIA (mwenye) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU
(ya nafsi) YAKE NAMOLA WAKO SI DHALIMU KWA WAJA WAKE."[41:46]
B: NAFASI YA SWALA KATIKA UIISLAM
Katka
kuonyesha umuhimu na nafasi ya swala,Bwana Mtume- Rehema na Amani
zimshukie –ameijaalia swala kuwa inashika nafasi ya pili katika nguzo
tano za uislam
"uislamu
umejengwa juu ya nguzo tano: kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye
kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah, kusimamisha swala,
kutoazakah, kufunga ramadhani na kuhiji Makkah-Mukaram" Bukhaariy.
Ukiitafakari
hadithi hii utaona ya kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie
–anaumathihsha uislamu na mfano wa jengo kubwa, imara na madhubuti
lililojengwa juu ya nguzo tano.
Hapana
hata mmoja awezaye kupinga kwamba kuna jengo linaloweza kusimama bila
ya nguzo. Kama tunakiri ukweli huu, basi ni dhahiri kwamba hapana uislam
pasipo na nguzo tano hizi na pasipo na nguzo na uislam pana kufru tu si
vinginevyo.
Eeh
Mola wetu tukinge na ukafiri kwa kutujulia kuisimamisha swala maisha
yetu yote Aamiyn. Inakupasa uelewe ewe nduguyangu mpenzi muislam kwamba
swala ndio nguzo tukufu kabisa ya dini na nafasi na umuhimu wa swala
katika uislamu ni kama vile ilivyo nafasi na umuhimu wa kichwa katika
kiwiliwili.
Basi
kama ambavyo asivyokuwa na uhai mtu asiye na kichwandivyo ambavyo hana
uislamumtu asiye na swala. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie
anatuasa kwa kutuambia :
"Ye yote atakuyeicha swala kwa makusudi, bila ya shaka amekufuru" Twabraaniy.
Haya hebu jiulize ewe Ndugu yangu Muislamu na uihurumie nafsi yako, mtu aliyekufuru ana Uislamu ?!
Fahamu
ewe Ndugu yangu unayemuasi Mola wako kwa kuacha kuswali kwamba sala
ndio nguzo ya dini hii, dini haipo bila ya nguzo hii. Haya
yanathibitishwa na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
"Swala ndio nguzo ya dini, atakayeisimamisha, hakika ameisimamisha dini na atakayeiacha, bila ya shaka huyo ameivunja dini".
Kwa
mantiki hii, mtu atakayeihifadhi nguzo hii kwa kuswali katika nyakati
zake maalumu na akatimiza sharti na nguzo zote hali kujinyenyekeza kwa
Mola wake na huku akiamini kuwa ni wajibu wake kuswali, huyo ndiye
atakayefaulu duniani na akhera. Tunasoma ndani ya Qur-ani Tukufu :
"KWA YAKINI WAMEFAULU WAUMINI AMBAO WAO NI WANYENYEKEVU KATIKA SWALA ZAO" Al-Muuminun : 1-2.
Kinyume
chake yule atakayeipuuzia swala, akaacha kuswali, huyo ndiye mtu muovu
aliyepata khasara duniani na akhera kwa sababu ya kuikhalifu amri ya
Mola Muumba wake.
Kwa
mujibu wa kauli iliyotangulia ya Bwana Mtume, wewe usiotaka kuliweka
paji lako la uso ardhini kumsujudia Mola wako umeichukua nyundo kubwa na
nzito unaivunja na kuibomoa dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Dini
ambayo amewatuma mitume wake wote, tangu Nabii Adam mpaka Mtume wa
mwisho Muhammad – Rehema na Amani ziwashukie wote – kuja kuisimamisha
katika katika ardhi hii. Je, mbomoa dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu si
mgomvi wa Allah, na hivi mtu anaweza kugombana na Allah kisha akatazamia
kupata salama ?! La hasha.
Ewe
mpenzi ndugu yangu, elewa na ufahamu kwamba swala ndiyo ibada ya kwanza
kabisa aliyoiwajibisha Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Amesema Bwana
Mtume – Rehema na Amani zimshukie - :
"Cha
mwanzo alichokifaradhisha Allah kwa umati wangu ni swala tano, na cha
mwanzo kinachorufaishwa (kinachopanda mbinguni) katika amali (matendo)
yao ni swala tano, na cha mwanzo watakachoulizwa katika amali zao ni
swala tano …."
Ndugu
yangu mpenzi usiotaka kumsujudia Mola wako aliyekuumba, haikutoshi
hadithi hii kuona ni jinsi gani ibada ya swala ilivyopewa umuhimu wa
kwanza katika Uislamu ?!
Amali
zako zote njema ni lazima zitanguliwe na swala tano ndipo zikubaliwe,
kinyume na hivyo amali hizo hazina maana bali ni sawa sawa na mavumbi
yapeperushwayo. Ushahidi wa haya ni kauli ya Bwana Mtume – Rehema na
Amani zimshukie –
"Cha
mwanzo atakachokaguliwa/atakachohesabiwa mja siku ya kiyama ni swala,
ikitengenea zimetengenea baki ya amali zake nyingine, ikifisidika
(swala) zimefisidika (zimeharibika) baki ya amali zake nyingine"
Ndugu mpenzi muislamu, ukiyakiri maneno haya ya Bwana Mtume yatakufikisha katika ukweli na hakika kwamba swala ndio ibada mama.
Kadhalika
ili kuonyesha utukufu wa ibada ya swala, utaikuta swala ndio ibada
pekee aliyoitiwa Bwana Mtume na kukabidhiwa na Mola wake mbinguni. Ibada
nyingine zote Bwana Mtume alikuwa akiletewa amri hapa hapa ardhini
kupitia kwa malaika Jibril – Amani imshukie – Allah alimkuhutubu Mtume
wake juu ya swala tano katika ule usiku wa Miraji pasina wasita wa
Jibril.
Amesema
Anas – Allah amridhie – Imefaradhishwa swala kwa Mtume – Rehema na
Amani zimshukie – usiku aliopelekwa mbinguni swala khamsini, kisha
zikapunguzwa mpaka zikawa tano, kisha (Mtume) akaitwa ewe Muhammad !
Hakika maneno yangu hayabadilishwi na utapata wewe katika swala tano
hizo ujira wa swala khamsini"
Ndugu yangu muislamu, hebu yatafakari kwa makini maneno ya Mtume wako, utauona utukufu wa ibada ya swala.
Ni
kwa ajili hiyo ndio tunaona Allah anatuamrisha kuhifadhi na kudumisha
swala na muislamu amewajibikiwa kuitekeleza swala muda wa kudumu roho
yake katika kiwiliwili chake.
Akiwa
mzima wa afya njema au mgonjwa asojiweza kitandani kwa sharti ya kuwa
na fahamu za kujua alitendalo. Awapo vitani au katika hali ya amani,
akiwa safarini au la, swala imemlazimu tu.
Mwanamume
na mwanamke wote ni sawa katika amri hii ya swala, ila mwanamke
hatoswali akiwa katika hali ya hedhi au nifasi. Amesema Mwenyezi Mungu
Mtukufu katika kuamrisha swala
"HIFADHINI
(angalieni sana) SWALA (zote kuziswali) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA
KATI NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABUDU ALLAH NA MKIWA KHOFU (
mmo vitani, basi swalini) HALI YA KUWA MNAKWENDA KWA MIGUU AU MMEPANDA
(wanyama) NA MTAKAPOKUWA KATIKA AMANI BASI MKUMBUKENI ALLAH (swalini)
KAMA ALIVYOKUFUNZENI YALE MLIYOKUWA HAMYAJUI" [2:238-239]
Ndugu yangu mpenzi, utabainikiwa kutokana na aya hii kwamba muislamu hana udhuru hata chembe unaomuhalalishia kuacha swala.
Hivyo
basi muislamu atakayeitekeleza swala kama itakikanavyo, swala hiyo
itakuwa ni hoja (wakili wa kumtetea) itakayomuokoa siku ya Kiyama, si
hivyo tu bali itakuwa ni nuru itakayomuangazia na kumuongoza katika siku
hiyo ngumu na nzito kama ambavyo itakovyokuwa ni sababu ya kufutiwa
madhambi yake.
Imepokelewa
kutoka kwa Sayyidna Uthman – Allah amuwie Radhi – amesema : nimemsikia
Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akisema :
"Hatawadhi mtu udhu wake vizuri kisha akaswali ila Allah humsamehe mtu huyo madhambi yaliyo baina ya swala hii na swala ijayo".
Basi
ni kheri na furaha iliyoje kwa yule aliyeitekeleza swala kwa ukamilifu,
ukamilifu na unyenyekevu mpaka anamaliza muda wake wa kuishi hapa
duniani (anakufa). Eh! Ole wake, tena ole wake na majuto yake yule
aliyefanya kibri, akaacha kuitekeleza swala hata akaondoka duniani bila
ya kumsujudia Mola wake. Hebu itegee sikio la usikivu kauli hii tukufu
ya Allah asema nini juu ya watu hawa :
"(Na
wawalete) HIYO SIKU KUTAKAYOKUWA NA MATESO MAKALI NA WATAITWA KUSUJUDU
LAKINI HAWATAWEZA. MACHO YAO YATAINAMIA CHINI; UNYONGE UTAWAFUNIKA NA
HAKIKA WALIKUWA WAKIITWA KUSUJUDU WALIPOKUWA SALAMA (na walikataa)"
[68:42-43].
Watu wa peponi watawauliza watu wa motoni :
"NI
KIPI KILICHOKUPELEKENI MOTONI ? WASEME : HATUKUWA MIONGONI MWA
WALIOKUWA WAKISWALI. HATUKUWA TUKILISHA MASIKINI. NA TULIKUWA TUKIZAMA
(katika maasia) PAMOJA NA WALIOKUWA WAKIZAMA" [74:42-45].
Khasara
na maangamivu yaliyoje, leo utawaona baadhi ya waislamu hawaswali na
hoja yao kubwa shughuli nyingi hawana nafasi, wametingwa na kazi na
wengine huthubutu hata kusema kwa kinywa kipana kabisa kwani ni lazima
kuswali, kama ninafanya mema mengine haitoshi ?! Hebu itegee sikio kauli
hii ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie - :
"Yeyote
yule atakayeihifadhi swala, iatkuwa (swala hiyo) ni nuru, hoja na
uokovu kwa mtu huyo siku ya Kiyama, na yeyote yule asiyeihifadhi swala,
haitokuwa (swala) ni nuru, hoja na uokovu kwa mtu huyo, bali atakuwa
(motoni) siku ya Kiyama pamoja na akina Qaarun, Fir-aun, Haaman na
Ubayyi bin Khalaf".
Fahamu
ewe ndugu yangu muislamu, swala ina nafasi na utukufu wa pekee katika
Uislamu ndio maana tunamkuta Bwana Mtume mara nyingi anatuhimiza swala
na swala ndio ulikuwa wasia wake wa mwisho wakati anaondoka duniani :
"Ninakuhimizeni na kukuusieni swala pamoja na wamilikiwa wa mikono yenu ya kuume".
C. KHATARI YA KUACHA SWALA
Ndugu
yangu Muislamu, bila shaka unatambua au umewahi kusikia kwamba Allah
aliwaamrisha malaika pamoja na Ibliis wamsujudie baba yetu Nabii Adam –
Amani imshukie – hali ya kumuamkia. Iblisi kwa ushupavu na kibri
alichokuwa nacho alikataa kuitii na kuitekeleza amri ya Mola wake.
Ni
kwa sababu hii tu Allah akamfukuza Iblis na kumtoa huko alikokuwa
pamoja na Malaika na akamlaani mpaka siku ya kiyama, na kesho akhera
ataingia motoni. Tusome kwa mazingatio :
"(na
wakumbushe watu khabari hii) TULIPOWAAMBIA MALAIKA MSUJUDIENI ADAM (
yaani mwadhimisheni kwa ile elimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA WOTE
ISIPOKUWA IBLIS, AKAKATAA NA AKAJIVUNA NA (toke hapo) ALIKUWA KATIKA
MAKAFIRI (ila tu alichanganyika tu na malaika)" [2:34].
Basi wewe ndugu yangu mpenzi usiotaka kuswali, hujioni kuwa wewe ni mbaya zaidi kuliko Iblis ?!
Iblis
alikataa kumsujudia Nabii Adam, wewe leo unakataa kumsujudia
aliyemuumba Nabii Adam. Iblis alikataa kusujudu mara moja tu, wewe leo
unakataa kusujudu mara thelathini na nne (34) kila siku, mara 238 kila
wiki, mara 1020 kila mwezi, mara 12,104 kwa mwaka, mara ….. katika umri
wako, jaza mwenyewe.
Iblis alikataa kusujudu sijida ya heshima kwa Nabii Adam, wewe unakataa kusujudu sijida ya ibada kwa Mola Muumba wako.
Hebu
angalia tena adhabu aliyopewa Iblis kwa kuacha sijida moja tu
alilaaniwa na kutolewa peponi na huku akisubiriwa kuliongoza kundi la
watu wa motoni kuingia motoni.
Hii
inamaanisha mwenye kuacha sijida 34 kila siku anastahiki kupata adhabu
kali zaidi ya ile aliyopewa Iblis mlaaniwa, sikwambii asioswali juma
moja au zaidi.
Ndugu
yangu usioswali unatarajia nini ikiwa hali ni hiyo ?! Unaona uzito gani
kumsujudia Mola wako ?! Aletwe Mtume mwingine ndio utasikia na kutii ?!
Hebu ihurumie nafsi yako, huiwezi adhabu ya Mola wako.
Ndugu
yangu umepewa neema ya akili, ishukuru neema hiyo kwa kuzingatia
uambiwayo, umepewa masikio ili usikie, isikie haki na kuifuata, usijitie
upofu na uziwi wa bure ukajuta na kuangamia. Zinduka, usiingie katika
kauli ya Allah isemayo :
"NA
BILA SHAKA TUMEWAUMBIA MOTO WA JAHANAMU WENGI KATIKA MAJINI NA WANADAMU
(kwa sababu hii): NYOYO WANAZO LAKINI HAWAFAHAMU KWAZO, NA MACHI WANAYO
LAKINI HAWAONI KWAYO, NA MASIKIO WANAYO LAKINI HAWASIKII KWAYO. HAO NI
KAMA WANYAMA, BALI WAO NI WAPOTOFU ZAIDI. HAO NDIO WALIOGHAFILIKA"
[7:179].
Tahadhari
ewe ndugu yangu, usiwe na sifa hizi zilizotajwa, kwani hizi ni sifa za
watu wabaya, watu wa motoni. Tumuombe Mola wetu Mtukufu asitujaalie kuwa
miongoni mwa watu wa motoni, wasiotaka kumsujudia – Amin.
0 comments:
Post a Comment