HUKUMU YA KUJICHUA..........ke/me join with ANGAZA & Alhidaaya

Lengo la ANGAZA ni kumwangazia yule anayefanya kitu akizania ni sahihi kumbe ni kuelekea katika ghadhabu za Mwenyezi Mungu.
 
Home
kabah
26 Swafar 1438 H

Nini Hukumu Ya Kujichua Sehemu Za Siri Au Kujisaga?

SWALI  LA KWANZA:
NAULIZA KWAMBA...DINI INASEMAJE KUHUSU KUPIGA PUNYETO KWA KIJANA AMBAYE BADO HAJAOA;NA HANAUWEZO  WAKUOA BADO
SWALI LA PILI:
as kum,  naomba kuuliza juu ya baadhi ya vijana wa kike na wa kiume,wanapofikia umri fulani au baada ya kubaleghe hujiwa na matamanio ya kujamii(sexual desires) hivyo wengine huamua kutoa manii kwa kutumia mikono yao na kwa wanawake huamua kujitia kitu chochote kinachoweza kuleta hisia na kupunguza matamanio yao.
 swali ni kwamba,je hadithi na quran inalizungumziaje swali hili.  natumai majibu mazuri.
SWALI LA TATU:
Assalam aleikum!                                  
 swali ni kuwa kujitoa
manii(nyeto) ni haramu au ni makuruu?kwani kwa fikra zangu naona ni vizuri kwani unapunguza matatamanio kwa wanawake na hasa kufanya tendo la zinaa kabla ya ndoa.



 
JIBU:
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah wasw-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  ‘Aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad
Hili ni swali muhimu kwa kuwa linagusa tatizo sugu linalowakabili vijana wengi wa Kiislam, ambao bado hawajaoa, na wanaokabiliana kwa hali ya juu kabisa na vishawishi vilivyowazunguka katika jamii mbalimbali wanazoishi ndani yake. Kujichua wanaume au kujisaga wanawake ni jambo linalokubalika na kufanyika sana katika jamii zisizo za Kiislam kwa idadi kubwa ya watu: vijana wa kiume na kike, makapera, wazee na hata waliooa/kuolewa.

Lakini hali hiyo katika Uislam ni kinyume. Kwani katika Uislam kujichua au kujisaga (punyeto) ni haraam kwa mwanamme na mwanamke, kwa dalili zifuatazo:
Kwanza, dalili kutoka katika Qur’aan:
((وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ))
 
 ((إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ))
 
 (( فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاء ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ))

((Na ambao wanazilinda tupu zao))
((Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa))
((Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka)) [Al-Muuminuun:5-7]
Aayah hii inakataza waziwazi vitendo vyote vya tendo la ndoa (ikijumuisha punyeto) isipokuwa kwa wake, na yeyote anayejipelekea kwenye matendo kinyume na hayo yaliyoruhusiwa, basi ni katika warukao mipaka.
وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّى يُغْنِيَهُمْ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ  
((Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu Awatajirishe kwa fadhila Yake)) [An-Nuur:33]
Ayah hii vilevile inaamrisha wazi kwa yule asiye na uwezo wa kimali kwa ajili ya kuoa, basi anatakiwa ajiweke katika hali ya kujidhibiti  na machafu na kujihifadhi kimwili na awe na subira ya kuweza kukabiliana na vishawishi mbalimbali ikiwemo kupiga punyeto, hadi Mwenyeezi Mungu Atakapomruzuku kwa fadhila Zake.

Vilevile Wanachoni wa Fiqh (Fuqahaa) wamechukulia hukumu kutoka katika ayah hii kuwa ni haraam kupiga punyeto kwa sababu mbili: Ya kwanza: Katika ayah hii, Allaah سبحانه وتعالى  Anaamrisha kujizuia na machafu, na kutokana na kanuni za ki-Fiqh, maamrisho  yanaashiria ulazima (uwajibu) wa jambo. Hivyo kubaki katika hali ya usafi (kujizuia na machafu) ni wajibu na panapokuwa kujizuia na machafu ni wajibu, basi kujizuia na yale yote yanayopelekea kufanya machafu ni wajibu zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba kujizuia na machafu au kubaki safi kutapatikana pale mtu anapojizuia na vile vyenye kusababisha hayo machafu.

Sababu ya pili, kwamba katika ayah hiyo Allaah سبحانه وتعالى    Ameamrisha Usafi (kutofanya machafu) kwa wale wasio na uwezo wa kuoa. Hapa Allaah سبحانه وتعالى Hajadhihirisha uhusiano wa kujizua na machafu na ule wa kuoa. Hivyo kunahesabika kuwa kujichua ni haraam. Na kama kungekuwa ni halaal, basi hapa ndipo pahala pake palipokuwa panatakikana kutajwa. Kwa kutotajwa uhalali wa kujichua katika ayah hii ambapo ndipo pahali muwafaka wa kuelezwa hilo, kunadhihirisha kuwa jambo hilo ni haraam, Kwani ‘kunyamazwa katika sehemu ya kuelezwa kunaashiria makatazo.’ Tazama pia tafsiri ya Imaam Qurtubiy katika ayah hiyo.

Pili, dalili kutoka katika Sunnah:
Anasema ‘Abdullaah ibn Mas’uud رضي الله عنه, “Tulikuwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na hali bado ni vijana na hatuna uwezo wa mali. Basi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  akatuambia: ((Enyi vijana! Mwenye kuweza kuoa na aoe, kwani kuoa kunamsaidia yeye kuinamisha macho yake (kutotazama ya haraam) na kuhifadhi tupu yake (kutofanya zinaa na uchafu mwingine), na yule asiye na uwezo wa kuoa, afunge, maana funga hupunguza matamanio ya kimwili)) Al Bukhaariy
Hadiyth hii inamuamrisha mtu asiye na uwezo wa kuoa, afunge, japokuwa kuna ugumu wa kufanya hivyo kila wakati anapozidiwa na matamanio, ili asitumbukie katika vitumbukizo vikiwemo punyeto, pamoja na urahisi na mvuto wa kulifanya jambo hilo. Na kama kungekuwa ni halali kupiga punyeto, basi hapa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  angeliruhusu kwa sababu ni jambo rahisi na lenye kustarehesha na asingesema watu wafunge kwani hilo ni jambo gumu na zito kulifanya. Na kama tunavyofahamu, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakuletwa kutufanyia ugumu na uzito.

Wema waliopita kama Sa’iyd ibn Jubayr رضي الله عنه anasema kuhusiana na punyeto, “Mwenyeezi Mungu Atawaadhibu watu kwa sababu walikuwa wakichezea sehemu zao za siri.” Naye ‘Atwaa  رحمه الله  anasema, “Baadhi ya watu watafufuliwa na hali mikono yao ina mimba, Nadhani ni wale waliokuwa wakipiga punyeto.”

Ingawa baadhi ya Maimam wanalijuzisha jambo hilo kwa sababu mbalimbali, kama; ikiwa mtu anaogopa kutumbukia katika zinaa, au kufanya huko ni kwa sababu tu ya kutoa matamanio yaliyozidi na wala si kwa ajili ya kujistarehesha n.k.. Hata hivyo, rai hizo hazina dalili yoyote zilizoambatana nazo, kwa hivyo ni bora mtu kujiepusha na tendo hilo kutokana na dalili zilizotangulia kutajwa.

Tunawanasihi ndugu zetu wenye kukabiliwa na vishawishi hivyo, wafuate nukta hizi ili ziwasaidie kupambana na hali hiyo inayowasumbua wale walio katika hali ya ukapera (kutokua na mke/mume):
1-    Jambo la mwanzo na muhimu kuliko yote ili kuepukana na mtihani huu wa kutumbukia katika tabia hiyo, ni kujitahidi kufuata maamrisho ya Allaah سبحانه وتعالى na kuogopa  adhabu Zake.

2-      Kuwa safi na machafu (Kujizuia na machafu), kwa kujiweka daima katika hali ya kufikiria adhabu ya moto, na kuamini kuwa kujihifadhi huko kwa kufanya machafu ni sababu ya kuipata pepo.

4-    Kuinamisha macho yako (kutotazama yale ya haraam kama picha za uchi, sinema, au kukaa majiani na kutazama maumbo ya wanawake wapitao). Kujizuia huko kutazama ya haraam, kutakusaidia sana kutoamsha hamu zilizorundikana ambazo zikishaamka, basi kufanyika haraam kunakuwa ni jambo lisiloepukika kirahisi. Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالى Ameamrisha wanaume na wanawake katika ayah mbili zifuatazo:
 
  ((وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ ))
((Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu Anazo khabari za wanayoyafanya))
((Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao….)) [An-Nuur:30-31] 
Naye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  anasema: ((Usifuatilize mtazamo (kuangalia kwa kutokusudia (vile vilivyoharamishwa) kwa mtazamo mwingine))[At-Tirmidhiy]
Huu ni mwongozo kutoka kwa Mtume wetu صلى الله عليه وآله وسلم wa kujizuia na yale yote yanayoweza kuchochea matamanio ya kimwili ambayo yanaweza kumpelekea mtu kufanya yaliyokatazwa.

5-    Ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo ni kukimbilia kuoa haraka pale tu unapokuwa tayari kiuwezo, kama tulivyoona katika hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   

6-   Kufunga. Jizoeshe kufunga kila unapohisi matamanio yanaanza kufumuka. Nako huko kufunga kunasaidia sana kwa mengi zaidi ya hilo. Jizoeshe kufunga kila Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe (tarehe 13, 14 na 15 za Kiislam, kila mwezi), na ukiona matamanio yako ni mengi na ya mara kwa mara basi funga Swawm ya Nabii Dawuud عليه السلام   ya kila baada ya siku moja.
        Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema:
))يَا مَعْشَرَ الشَّبَابِ مَنْ اسْتَطَاعَ الْبَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ وَأَحْصَنُ لِلْفَرْجِ وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَعَلَيْهِ بِالصَّوْمِ فَإِنَّهُ لَهُ وِجَاءٌ((  البخاري ومسلم
((Enyi vijana, anayeweza kuoa basi na aoe kwani ni kuinamisha macho na ni stara ya uchi, Na asiyeweza basi afunge (Swawm) kwani ni kinga (ya matamanio).[Al-Bukhaariy na Muslim]

7.    Kuutumia muda wako usio na la kufanya, kwa kufanya ibada zaidi na kujisomea na kutafuta elimu ya dini; kwa kusikiliza mawaidha au kutazama.

8.    Kujiepusha na kutumia baadhi ya vyakula, vinywaji n.k. ambavyo vinachochea hamu na kusababisha mshawasha na muibuko wa matamanio.

9.    Daima fikiria madhara yanayoweza kusababishwa na tendo hilo; kama ya kudhoofisha nguvu za macho, nguvu za mishipa, nguvu za uume (kwa mwanamme) au uti wa mgongo. Na muhimu zaidi, ni kule kuwa na hisia za dhambi na usumbufu utakaopatikana baada ya kufanya kitendo hicho kama vile, kuweza kupoteza Swalah ya faradhi kwa kukubidi kuchukua muda wa kwenda kuoga kila baada ya tendo hilo.

10.   Fanya Tawbah, muombe Allaah سبحانه وتعالى  msamaha kila wakati, kufanya hivyo na pia kutenda matendo mema na kutokata tamaa na Rahma za Allaah سبحانه وتعالى   kunaweka karibu zaidi na Allaah سبحانه وتعالى na kukufanya kumuogopa zaidi na kufikiria kila tendo unalotaka kulifanya kwanza.

11.   Jua kuwa Allaah سبحانه وتعالى ni Mwingi wa Kusamehe na daima Humkubalia du’aa za yule anayemtaka msaada. Hivyo basi, kumuomba Allaah سبحانه وتعالى msamaha ni jambo lenye kupokelewa Naye, na hilo linatupa nguvu kumuomba Yeye daima na kutaraji msamaha Wake.

12.  Kujishughulisha na mambo ya muhimu na ya faida; yakiwa ni ya akhera au ya kilimwengu ili usipate nafasi ya kuwa na faragha na ukaanza kufikiria kufanya tendo hilo ambalo hakika ni ada iliyo ngumu kuepukika.

13.   Fanya mazoezi mbalimbali ya kukuchosha, mwili ukishachoka matamanio yanazama.

14.  Usile sana, au kula kila wakati. Kwani unaposhiba mambo mengine yanachemka na kutaka haki zake.

Hayo ndio machache katika mengi ambayo yanaweza kumsaidia mtu kujiweka mbali na tendo hilo linalowasumbua wengi haswa vijana na wajane.

Wa Allaahu A’alam

Share on Google Plus

About DAIMA ANGAZA

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment