ULIMWENGU HUU MBONA UNAENDESHWA NA RIBA??????



2. SURA AL- BAQARA

(Imeteremka
Madina)



Sura hii imeteremka Madina baada ya Hijra. Nayo ndiyo sura
ndefu kuliko zote katika Qur'ani Tukufu kwa mujibu wa mtungo wa Msahafu.



Sura hii imeanzia kueleza kwa tafsili yale yaliyo malizikia
Sura ya Al Faatiha. Imetaja kuwa Qur'ani ndiyo msingi wa uwongofu, na imewataja
wale walio neemeshwa na Mwenyezi Mungu kwa kupata radhi zake, na wale walio
kasirikiwa, nao ni makafiri na wanaafiki.



Sura imeeleza ukweli wa Qur'ani, na kwamba wito wake ni wa
kweli usio na shaka. Kisha ikaingia kueleza namna tatu za watu: Waumini,
Makafiri na Wanaafiki. Na ikataja Daa'wa, Mlingano, au Wito, kuwaita watu
wamuabudu Mwenyezi Mungu pekee, na ikawaonya makafiri, na ikawapa bishara njema
Waumini. Baadaye ikawaelekea Wana wa Israili khasa kwa kuwaita na kuwakumbusha
siku za Mwenyezi Mungu, na kwa vituko vyao na Musa a.s. na kuwakumbusha khabari
za Ibrahim na Ismail na walivyo ijenga Al Kaaba. Hayo yamechukua karibu nusu ya
Sura. Mazungumzo yakawageukia Waumini wazingatie yaliyo wapata Mayahudi na
Wakristo.



Mazungumzo yakaingia kuwasemeza watu wa Qur'ani kwa kuwakumbusha mambo ambayo
umma wa Musa na umma wa Muhammad walivyo shirikiana katika kutukuzwa Ibrahim na
kuongoka kwake na nasaba yake, na kwa kutaja kibla na mfano wa hayo.



Kisha yakaja mazungumzo juu ya Tawhid (Upweke wa Mwenyezi
Mungu) na kukumbusha Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kumuashiria Yeye. Na yakaja
masimulizi juu ya ushirikina, na juu ya vyakula vilivyo harimishwa, na kwamba
kuharimisha na kuhalalisha ni haki ya Mwenyezi Mungu peke yake.



Sura ikaingia kubainisha misingi ya wema, na kutaja baadhi
ya hukumu za Saumu, na wasia, na kula mali ya watu kwa dhulma, na kisasi, na
vita, na Hija, na ulevi, na kamari, na ndoa na talaka, na kunyonyesha, na eda
na mengineyo. Hali kadhaalika yamezungumzwa mambo ya itikadi kwa jumla kama
Utume, Tawhidi, kufufuliwa. Yametajwa mas-ala ya kutoa sadaka na Zaka, riba,
biashara, kuandikiana madeni.



Mwishoe Sura yakhitimisha kwa dua ya Waumini kumwomba Mola
wao Mlezi awanusuru na awasaidie.

Sura hii imekusanya misingi kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwayo
ni:

Kwamba Njia ya Mwenyezi Mungu na kuishika Dini yake ni
dharura kwa ajili ya kupata mafanakio duniani na Akhera, na kwamba haielekei
kwa mwenye akili kuwaita watu watende mema naye akajisahau mwenyewe; na ya
kwamba yapasa kuchagua kheri kuliko shari, na kukhiari lilio bora kuliko lilio
duni.



Na kwamba misingi ya Dini ni mitatu, nayo ni: Kumuamini
Mwenyezi Mungu, Kuamini kufufuliwa, na Kutenda mema.



Na kwamba malipo ni kwa Imani na vitendo pamoja. Shuruti ya
Imani ni kukiri kwa nafsi na kukubali kwa moyo kila alilo kuja nalo Mtume
s.a.w., na kwamba wasio kuwa Waislamu hawatokuwa radhi na Waislamu mpaka
Waislamu wafuate dini yao hao walio potea.



Na kwamba kwa jumla urafiki katika sharia yapasa uwe kwa
wenye kushika Imani na uadilifu, sio kwa watu wa kufuru na dhulma, na kwamba
Imani ya Dini ya Mwenyezi Mungu inalazimisha uwepo umoja na kuwafikiana, na
kutofuata hayo huleta khitilafu na kutengana. Kwa ajili ya kupata mambo makuu
inalazimu kutafuta msaada kwa Subira na Sala. Kufuata kipofu-pofu ni upotovu,
na hupelekea ujinga na chuki za kitaifa.



Na kwamba Mwenyezi Mungu amewahalalishia waja wake vyakula
vizuri na amewaharimishia vichache vilivyo viovu; wala haijuzu kwa asiye kuwa
Mwenyezi Mungu kuhalalisha au kuharimisha kitu. Na vilivyo harimishwa
huhalalishiwa mwenye dharura, kwa sababu dharura huruhusu vilivyo katazwa, na
dharura hupimwa kwa kadiri yake. Dini imejengwa juu ya wepesi na kuondoa mikazo.
Kwani Mwenyezi Mungu hailazimishi nafsi ila kwa kiasi ya uwezo wake, wala
hawaamrishi waja wake ila kwa wanalo liweza. Ni haramu, haijuzu mtu kujipelekea
nafsi yake kwenye maangamizo. Kila jambo hutafutwa kwa sababu zake na njia zake
zitakao fikilia. Kulazimisha katika dini kunakatazwa. Kupigana vita ni kwa
ajili ya kujilinda, na kwa ajili ya kuhifadhi uhuru wa dini, na kuulinda
utukufu wa Uislamu katika miji yake.



Na kwamba Muislamu anayo haki ya kutaka sehemu yake katika
dunia, kama anavyo tekeleza wajibu wake kwa ajili ya Akhera, na kwamba kutimiza
haja na kuleta maslaha ni miongoni mwa makusudio ya Sharia.



Na kwamba Imani na Subira ni sababu mbili zinazo wapelekea
wachache walio waadilifu kuwashinda wengi wenye kudhulumu, na kula mali ya watu
kwa upotovu ni haramu, na mwanaadamu analipwa kwa vitendo vyake mwenyewe si kwa
vitendo vya mwenginewe, na hikima ya utungaji sharia inafahamiwa na akili iliyo
kaa sawa kwa kuwa ndani yake mna haki na uadilifu na maslaha ya waja.






KWA
JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1.
Alif Lam Mim.
Maelezo

2.
Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu,
Maelezo

3.
Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika tuliyo wapa.
Maelezo

4.
Na ambao wanayaamini yaliyo teremshwa kwako, na yaliyo teremshwa kabla yako; na
Akhera wana yakini nayo.

Maelezo

5.
Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio walio fanikiwa.
Maelezo

6.
Hakika wale walio kufuru ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawaamini.
Maelezo

7.
Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao, na juu ya
macho yao pana kifuniko. Basi watapata adhabu kubwa.
Maelezo

8.
Na katika watu, wako wasemao: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho,
wala wao si wenye kuamini.

Maelezo

9.
Wanatafuta kumdanganya Mwenyezi Mungu na wale walio amini, lakini hawadanganyi
ila nafsi zao; nao hawatambui.

Maelezo
10. Nyoyoni mwao mna maradhi, na
Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu
ya kusema kwao uwongo.
Maelezo
11.
Na wanapo ambiwa: Msifanye uharibifu ulimwenguni. Husema: Bali sisi ni
watengenezaji.
Maelezo
12.
Hakika wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.
Maelezo

13.
Na wanapo ambiwa: Aminini kama walivyo amini watu. Husema: Tuamini kama walivyo
amini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini hawajui tu.
Maelezo

14.
Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao na
mashet'ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki
tu.
Maelezo

15.
Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawawacha katika upotofu wao wakitangatanga
ovyo.
Maelezo

16.
Hao ndio walio nunua upotofu kwa uwongofu; lakini biashara yao haikupata tija,
wala hawakuwa wenye kuongoka.

Maelezo

17.
Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto, na ulipo tanda mwangaza wake kote
kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha katika giza, hawaoni.
Maelezo

18.
Viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.
Maelezo

19.
Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na radi na umeme; wakawa
wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na
Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.

Maelezo

20.
Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea mwangaza huenda, na unapo
wafanyia giza husimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu angeliondoa kusikia kwao
na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Maelezo

21.
Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni nyinyi na wale wa kabla
yenu, ili mpate kuokoka.

Maelezo

22.
(Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu
kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe
riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua.
Maelezo

23.
Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya
mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema
kweli.
Maelezo

24.
Na mkitofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake
ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha.
Maelezo

25.
Na wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo
mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo
pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio
takasika; na wao humo watadumu.

Maelezo

26.
Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake.
Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao
Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu
kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini
hawapotezi ila wale wapotovu,

Maelezo

27.
Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyo
amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio
wenye khasara.
Maelezo

28.
Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu akakufufueni! Kisha
atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?.
Maelezo

29.
Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi. Tena akazielekea
mbingu, na akazifanya mbingu saba. Naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.
Maelezo

30.
Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi
Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na
kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu
wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua.
Maelezo

31.
Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na
akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.
Maelezo

32.
Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza
Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.
Maelezo

33.
Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema:
Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua
mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?
Maelezo

34.
Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis,
alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.
Maelezo

35.
Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo
maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale
walio dhulumu.
Maelezo

36.
Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyo kuwamo, na
tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa
makaazi yenu na starehe kwa muda.

Maelezo

37.
Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia
toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.
Maelezo

38.
Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uwongofu utokao kwangu, basi
watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
Maelezo

39.
Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu, hao ndio watakao kuwa watu wa
Motoni, humo watadumu.
Maelezo

40.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo kuneemesheni, na timizeni
ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na niogopeni Mimi tu.
Maelezo

41.
Na aminini niliyo yateremsha ambayo yanasadikisha mliyo nayo, wala msiwe wa
kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa thamani ndogo. Na niogopeni Mimi
tu.
Maelezo

42.
Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha kweli nanyi mnajua.
Maelezo

43.
Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanao inama.
Maelezo

44.
Je! Mnawaamrisha watu mema na mnajisahau nafsi zenu, na hali nyinyi mnasoma
Kitabu? Basi je, hamzingatii?

Maelezo

45.
Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu
isipokuwa kwa wanyenyekevu,

Maelezo

46.
Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika
watarejea kwake.
Maelezo

47.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni zile neema zangu nilizo kuneemesheni, na
nikakuteuweni kuliko wote wengineo.

Maelezo

48.
Na iogopeni Siku ambayo mtu hatomfaa mtu kwa lolote, wala hayatakubaliwa kwake
maombezi, wala hakitapokewa kikomboleo kwake; wala hawatanusuriwa.
Maelezo

49.
Na vile tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya,
wakiwachinja wana wenu wa kiume na wakawawacha hai wanawake; na katika hayo
ulikuwa ni mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola wenu Mlezi.
Maelezo

50.
Na tulipo ipasua bahari kwa ajili yenu na tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa
Firauni, na huku mnatazama.

Maelezo

51.
Na tulipo muahidi Musa masiku arubaini, kisha mkachukua ndama (mkamuabudu)
baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.

Maelezo

52.
Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate kushukuru.
Maelezo

53.
Na tulipo mpa Musa Kitabu na pambanuo ili mpate kuongoka.
Maelezo

54.
Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu
nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na
ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu. Naye akapokea toba
yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba na Mwenye kurehemu.
Maelezo

55.
Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi.
Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia.

Maelezo

56.
Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru.
Maelezo

57.
Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni Manna na Salwa;
tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyo kuruzukuni. Nao hawakutudhulumu
Sisi lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao.
Maelezo

58.
Na tulipo sema: Ingieni mji huu, na humo mle mpendapo maridhawa, na ingieni
katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni: Tusamehe! Tutakusameheni makosa
yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
Maelezo

59.Lakini
walio dhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa waliyo ambiwa. Kwa hivyo
tukaiteremsha juu ya wale walio dhulumu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya
walivyo kuwa wamepotoka.

Maelezo

60.
Na Musa alipo omba maji kwa ajili ya watu wake, tulimwambia: Lipige jiwe kwa
fimbo yako. Mara zikatimbuka chemchem kumi na mbili; kila kabila ikajua mahali
pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe riziki ya Mwenyezi Mungu, wala
msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.

Maelezo

61.
Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi
tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea katika ardhi, kama mboga
zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema:
Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo
viomba. Na wakapigwa na unyonge,na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya
Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi
Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na
wakapindukia mipaka.
Maelezo

62.
Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini
Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa
Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Maelezo

63.
Na tulipo chukua ahadi yenu, na tukaunyanyua mlima juu yenu (tukakwambieni):
Shikeni kwa nguvu haya tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili
mpate kujilinda.
Maelezo

64.
Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu
na rehema zake, mngeli kuwa miongoni mwa wenye kukhasirika.
Maelezo

65.
Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni mwenu walio ivunja Sabato,(siku ya
mapumziko, Jumaa Mosi) na tukawaambia: Kuweni manyani wadhalilifu.
Maelezo

66.
Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale walio kuwa katika zama zao na
walio kuja baada yao, na mawaidha kwa wachamngu.
Maelezo

67.
Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje
ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa
Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.
Maelezo

68.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni ng'ombe gani? Akasema:
Hakika Yeye anasema kwamba ng'ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa
katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.
Maelezo

69.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini rangi yake? Akasema: Yeye
anasema, kuwa ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza
wanao mtazama.
Maelezo

70.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona
ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda,
tutaongoka.
Maelezo

71.
Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni ng'ombe asiye tiwa kazini kulima ardhi wala
kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja,
na walikaribia kuwa wasifanye hayo.

Maelezo

72.
Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye
kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha.

Maelezo

73.
Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng'ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu
huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili mpate kufahamu.
Maelezo

74.
Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, hata zikawa kama mawe au ngumu
zaidi; kwani kuna mawe yanayo timbuka mito, na kuna mengine yanayo pasuka
yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa sababu ya khofu ya
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yafanya.
Maelezo

75.
Mnatumai watakuaminini na hali baadhi yao walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi
Mungu, kisha wakayabadili baada ya kuwa wameyafahamu, na hali wanajua?
Maelezo

76.
Na wanapo kutana na wale walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke
yao, wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyo kufunulieni Mwenyezi Mungu ili
wapate kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi? Basi hamfahamu nyinyi?
Maelezo

77.
Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza?
Maelezo

78.
Na wako miongoni mwao wasio jua kusoma; hawakijui Kitabu isipo kuwa uwongo
wanao utamani, nao hawana ila ni kudhania tu.
Maelezo

79.
Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka
kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo
andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo yachuma.
Maelezo

80.
Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa
Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au
mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua?
Maelezo

81.
Naam, anaye chuma ubaya - na makosa yake yakamzunguka - hao ndio watu wa
Motoni; humo watadumu.
Maelezo

82.
Na wale walio amini na wakatenda mema, hao ndio watu wa Peponi, humo watadumu.
Maelezo

83.
Na tulipo funga agano na Wana wa Israili: Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi
Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na
watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa
wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.
Maelezo

84.
Na tulipo chukua agano lenu kuwa hamtamwaga damu zenu, wala hamtatoana
majumbani mwenu; nanyi mkakubali nanyi mnashuhudia.
Maelezo

85.
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani kwao,
mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka mnawakomboa, na hali
kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi
hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya
duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi
Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda.
Maelezo

86.
Hao ndio walio nunua uhai wa dunia kwa (uhai wa) Akhera; kwa hivyo
hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.
Maelezo

87.
Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na
tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho
Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi
zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.
Maelezo

88.
Na walisema: Nyoyo zetu zimefunikwa. Bali Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru
zao: kwa hivyo ni kidogo tu wanayo yaamini.
Maelezo

89.
Na kilipo wajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha waliyo
nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi kuwashinda makafiri - yalipo wajia
yale waliyo kuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu juu ya
wakanushao!
Maelezo

90.
Kiovu kweli walicho jiuzia nafsi zao, nacho ni kule kukataa kwao aliyo
yateremsha Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kuona maya kwa kuwa Mwenyezi Mungu
humteremshia fadhila yake amtakaye miongoni mwa waja wake. Basi wamejiletea
wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu. Na makafiri watapata mateso ya kudhalilisha.
Maelezo

91.
Na wanapo ambiwa: Yaaminini aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu. Wao husema:
Tunaamini tuliyo teremshiwa sisi. Na huyakataa yasiyo kuwa hayo. Na hali ya
kuwa hii ndiyo Haki inayo thibitisha yale waliyo nayo wao. Sema: Mbona mliwauwa
Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani ikiwa kweli mlikuwa Waumini?
Maelezo

92.
Na alikufikieni Musa na hoja zilizo waziwazi, kisha mkamchukua ndama
(kumuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
Maelezo

93.
Na tulipo chukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu (tukakwambieni):
Kamateni kwa nguvu haya tuliyo kupeni na sikieni. Wakasema: Tumesikia na
tumekataa! Na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya) ndama kwa kufuru yao. Sema:
Ni uovu mno iliyo kuamrisheni imani yenu ikiwa ni wenye kuamini.
Maelezo

94.
Sema: Ikiwa nyumba ya Akhera iliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni yenu tu bila ya watu
wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi mnasema kweli.
Maelezo

95.
Wala hawatayatamani kamwe kwa sababu ya yale yaliyo tangulizwa na mikono yao;
na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema wanao dhulumu.
Maelezo

96.
Na hakika utawaona ni wenye kuwashinda watu wote kwa pupa ya kuishi, na kuliko
washirikina. Kila mmoja wao anatamani lau angeli pewa umri wa miaka elfu. Wala
hayo ya kuzidishiwa umri hayamuondoshei adhabu; na Mwenyezi Mungu anayaona
wanayo yatenda.
Maelezo

97.
Sema: Aliye kuwa ni adui wa Jibril, basi huyo ndiye aliye iteremsha Qur'ani
moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, inayo thibitisha yaliyo kuwa kabla
yake, na ni uwongofu na bishara njema kwa Waumini.
Maelezo

98.
Aliye kuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibril na
Mikail, basi hakika Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.
Maelezo

99.
Hakika tumekuteremshia Ishara zilizo wazi na hapana wanao zikataa ila wapotovu.
Maelezo

100.
Je! Ati ndio kila wanapo funga ahadi huwapo kikundi miongoni mwao kikaivunja?
Bali wengi wao hawaamini.

Maelezo

101.
Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo
nayo, kundi moja miongoni mwa wale walio pewa Kitabu lilitupa Kitabu cha
Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.
Maelezo

102.
Na wakafuata yale waliyo zua mashet'ani kuuzulia ufalme wa Su leiman. Na wala
Suleiman hakukufuru, bali mashet'ani ndio walio kufuru, wakiwafundisha watu
uchawi, na yaliyo teremshwa kwa Malaika wawili, Haaruta na Maaruta katika
Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni
mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na
mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza
yatayo wadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika wanajua kwamba aliye khiari haya
hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walicho jiuzia
nafsi zao laiti wangelijua.

Maelezo

103.
Na lau kuwa wangeamini na wakaogopa, bila ya shaka malipo yatokayo kwa Mwenyezi
Mungu yange kuwa bora. Laiti wangeli kuwa wanajua!
Maelezo

104.
Enyi mlio amini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni: "Ndhurna".
Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
Maelezo

105.
Walio kufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina hawapendi mteremshiwe
kheri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa
rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
Maelezo

106.
Ishara yoyote tunayo ifuta au tunayo isahaulisha tunailetea iliyo bora kuliko
hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu?
Maelezo

107.
Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na ardhi? Nanyi hamna mlinzi
wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
Maelezo

108.
Au mnataka kumwomba Mtume wenu kama alivyo ombwa Musa zamani? Na anaye
badilisha Imani kwa ukafiri bila ya shaka huyo ameipotea njia iliyo sawa.
Maelezo

109.
Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wange kurudisheni nyinyi muwe
makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi
zao, baada ya kwisha wapambanukia Haki. Basi sameheni na wachilieni mbali mpaka
Mwenyezi Mungu atapo leta amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila
kitu.
Maelezo

110.
Na shikeni Sala na toeni Zaka; na kheri mtakazo jitangulizia nafsi zenu
mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yafanya.
Maelezo

111.
Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Yahudi au Mkristo. Hayo ni
matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni wasema kweli.
Maelezo

112.
Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu naye ni mtenda
mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao
wala hawatahuzunika.
Maelezo

113.
Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo. Na Wakristo husema: Mayahudi
hawana lao jambo. Na ilhali wote wanasoma Kitabu hicho hicho (Biblia). Na
kadhaalika walisema wale wasio jua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi
Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa
wakikhitilafiana.
Maelezo

114.
Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye zuia misikiti ya Mwenyezi Mungu
kutajwa ndani yake jina lake na akajitahidi kuiharibu? Watu hao haitawafalia
kuingia humo ila nao wanaogopa. Duniani watapata hizaya na Akhera watapata
adhabu kubwa.
Maelezo

115.
Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnako elekea, huko
Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa na Mjuzi.
Maelezo

116.
Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu! Ametakasika na hayo. Bali
vyote viliomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote vinamt'ii Yeye.
Maelezo

117.
Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na anapo taka jambo basi
huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.

Maelezo

118.
Na walisema wale wasio jua kitu: Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au
zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale walio kuwa kabla yao mfano wa
kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi Ishara kwa
watu wenye yakini.
Maelezo

119.
Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri, na mwonyaji. Na wala hutaulizwa
juu ya watu wa Motoni.
Maelezo

120.
Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika
uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada
ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu.
Maelezo

121.
Wale tulio wapa Kitabu, wakakisoma kama ipasavyo kusomwa, hao ndio kweli
wanakiamini. Na wanao kikataa basi hao ndio wenye kukhasiri.
Maelezo

122.
Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyo kuneemesheni, na hakika Mimi
nikakufadhilisheni kuliko wengineo wote.
Maelezo

123.
Na iogopeni siku ambayo hatamfaa mtu mwenziwe kwa lolote, wala hakitakubaliwa
kwake kikomboleo, wala maombezi hayatamfaa, wala hawatanusuriwa.
Maelezo

124.
Na Mola wake Mlezi alipo mjaribu Ibrahim kwa kumpa amri fulani, naye
akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi wa watu. Akasema:
Je, na katika vizazi vyangu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye
kudhulumu.
Maelezo

125.
Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia
watu na pahala pa amani. Na alipo kuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa
kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya
wanao izunguka kwa kut'ufu na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na
kusujudu.
Maelezo

126.
Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na
uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza
kwenye adhabu ya Moto, napo ni pahala pabaya mno pa kurejea.
Maelezo

127.
Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba:
Ewe Mola Mlezi wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe ndiye Msikizi Mjuzi.
Maelezo

128.
Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa
vizazi vyetu wawe umma ulio silimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na
utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Maelezo

129.
Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anaye tokana na wao, awasomee Aya zako, na
awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu,
Mwenye hikima.
Maelezo

130.
Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipo kuwa anayeitia nafsi yake katika
upumbavu? Na kwa yakini Sisi tulimteuwa yeye katika dunia; na hakika yeye
katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
Maelezo

131.
Na Mola wake Mlezi alipo mwambia: Silimu, Nyenyekea! Alinena: Nimesilimu,
nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu wote.
Maelezo

132.
Na Ibrahim akawausia wanawe, na pia Yaaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu
amekuteulieni Dini hii; basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu.
Maelezo

133.
Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani
baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na
Ismail na Is- hak, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.
Maelezo

134.
Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata waliyo yachuma, nanyi mtapata mtakayo
yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyo kuwa wakiyafanya wao.
Maelezo

135.
Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio mtaongoka. Sema: Bali tunashika
mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina.
Maelezo

136.
Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na
yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na
waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao
Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.
Maelezo

137.
Basi wakiamini kama mnavyo amini nyinyi, itakuwa kweli wameongoka. Na
wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi Mungu atakutosheni
kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye Msikizi, Mjuzi.
Maelezo

138.
Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu, na nani aliye mbora wa kupaka rangi
kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu Yeye tu.
Maelezo

139.
Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni Mola wetu Mlezi na Mola
wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi
tunamsafia Yeye tu.
Maelezo

140.
Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zao walikuwa
Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni
nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliye ficha ushahidi alio nao utokao
kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na hayo myafanyayo.
Maelezo

141.
Hao ni watu walio kwisha pita. Wao watapata waliyo yachuma, na nyinyi mt apata
mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyo kuwa wakifanya wao.
Maelezo

142.
WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilicho wageuza kutoka kibla chao
walicho kuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu;
Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyo nyooka.
Maelezo

143.
Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya
watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulicho kuwa
nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea
nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani
Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu.
Maelezo

144.
Kwa yakini tukiona unavyo geuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza
kwenye Kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na
popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo; na hakika wale walio pewa
Kitabu wanajua kwamba hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi
Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayo yatenda.
Maelezo

145.
Na hao walio pewa Kitabu, hata ukiwaletea hoja za kila namna, hawatafuata Kibla
chako; wala wewe hutafuata kibla chao, wala baadhi yao hawatafuata kibla cha
wengineo; na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya kukufikia ujuzi, hakika
hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhullumu.
Maelezo

146.
Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao; na kuna
kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.
Maelezo

147.
Haki inatoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wanao fanya shaka.
Maelezo

148.
Na kila mmoja anao upande anao elekea. Basi shindanieni mema. Popote mlipo
Mwenyezi Mungu atakuleteni nyote pamoja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa
kila kitu.
Maelezo

149.
Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na hiyo ndiyo Haki
itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo
yatenda.
Maelezo

150.
Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na popote mlipo
elekezeni nyuso zenu upande huo ili watu wasiwe na hoja juu yenu, isipokuwa
wale walio dhulumu miongoni mwao. Basi msiwaogope wao, lakini niogopeni Mimi -
na ili nikutimizieni neema yangu, na ili mpate kuongoka.
Maelezo

151.
Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na nyinyi, anakusomeeni Aya zetu na
kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima na kukufundisheni mliyo kuwa
hamyajui.
Maelezo

152.
Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru.
Maelezo

153.
Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu yu
pamoja na wanao subiri.

Maelezo

154.
Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti; bali
hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui.

Maelezo

155.
Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali
na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri,
Maelezo

156.
Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake
Yeye hakika tutarejea.
Maelezo

157.
Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio
wenye kuongoka.
Maelezo

 
158.
Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye
hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye
jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na
Mjuzi.
Maelezo

159.
Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha -- nazo ni hoja zilizo wazi na
uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni -- hao anawalaani
Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.
Maelezo

160.
Ila wale walio tubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba
yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
Maelezo

161.
Hakika walio kufuru na wakafa hali ni makafiri, hao iko juu yao laana ya
Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.
Maelezo

162.
Watadumu humo. Hawata-punguziwa adhabu wala hawatapewa muda wa kupumzika.
Maelezo

163.
Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema,
Mwenye kurehemu.
Maelezo

164.
Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana,
na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo
yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada
ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya
pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka
zimo Ishara kwa watu wanao zingatia.

Maelezo

165.
Na katika watu wapo wanao chukua waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda
kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu
zaidi sana. Na laiti walio dhulumu wakajua watakapo iona adhabu kuwa nguvu zote
ni za Mwenyezi Mungu na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!
Maelezo

166.
Walio fuatwa watakapo wakataa wale walio wafuata, na hali ya kuwa wamekwisha
iona adhabu; na yatakatika mafungamano yao.
Maelezo

167.
Na watasema wale walio fuata: Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama
wanavyo tukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyo waonyesha vitendo
vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni.
Maelezo

168.
Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo
za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhaahiri.
Maelezo

169.
Yeye anakuamrisheni maovu na machafu, na mumsingizie Mwenyezi Mungu mambo msiyo
yajua.
Maelezo

170.
Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali
tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa
hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?

Maelezo

171.
Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa anaye mpigia kelele asiye sikia ila
wito na sauti tu -- ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi.
Maelezo

172.
Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi
Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.

Maelezo

173.Yeye
amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilicho tajiwa,
katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliye fikiwa
na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Maelezo

174.
Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu, wakanunua
kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipo kuwa moto, wala Mwenyezi
Mungu hatawasemeza Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa. Nao watapata adhabu
chungu.
Maelezo

175.
Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu, na adhabu badala ya maghfira.
Ama wavumilivu wa Moto watu hawa!

Maelezo

176.
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki. Na wale walio
khitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki.
Maelezo

177.
Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema
ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na
Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na
wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa
Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na
dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.
Maelezo

178.Enyi
mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika walio uwawa - muungwana kwa
muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na
ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani.
Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye
vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.
Maelezo

179.
Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike.
Maelezo

180.
Mmeandikiwa -- mmoja wenu anapo fikwa na mauti, kama akiacha mali -- afanye
wasia kwa wazazi wake na jamaa zake kwa namna nzuri inayo pendeza. Ni waajibu
haya kwa wachamngu.
Maelezo

181.
Na atakaye ubadilisha wasia baada ya kuusikia, basi dhambi yake ni juu ya wale
watakao ubadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Maelezo

182.
Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo au kupata dhambi akasuluhisha baina
yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye
kurehemu.
Maelezo

183,
Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu
ili mpate kuchamngu.
Maelezo

184.
(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au
yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza,
watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi
ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.
Maelezo

185.
Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu,
na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika
mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu
katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala
hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu
kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.
Maelezo

186.
Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu.
Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini
Mimi, ili wapate kuongoka.

Maelezo

187.
Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na
nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi
zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa
changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na
kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha
timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini.
Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu
anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.
Maelezo

188.
Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula
sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.
Maelezo

189.
Wanakuuliza khabarai ya miezi. Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya
watu na Hija. Wala sio wema kuziingia nyumba kwa nyuma. Bali mwema ni mwenye
kuchamngu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili
mpate kufanikiwa.
Maelezo

190.
Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze
uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui.
Maelezo

191.
Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote walipo kutoeni; kwani fitina ni
mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka
wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo
yalivyo malipo ya makafiri.

Maelezo

192.
Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Maelezo

193.
Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na
kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa wenye kudhulumu.
Maelezo

194.
Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi. Anaye
kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri alivyo kushambulieni. Na mcheni
Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
Maelezo

195.
Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika
maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
Maelezo

196.
Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mkizuiwa,basi
(chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka
wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi
kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja
wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra
kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata,
afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili.
Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu.
Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Maelezo

197.
Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi
asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika
Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua. Na jitengezeeni
zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na nicheni Mimi, enyi wenye
akili!
Maelezo

198.
Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola wenu Mlezi. Na mtakapo miminika
kutoka A'rafat mtajeni Mwenyezi Mungu penye Masha'ril Haram. Na mkumbukeni kama
alivyo kuongoeni, ijapo kuwa zamani mlikuwa miongoni mwa walio potea.
Maelezo

199.
Kisha miminikeni kutoka pale wanapo miminika watu, na muombeni Mwenyezi Mungu
msamaha: hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Maelezo

200.
Na mkisha timiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa
mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya watu wanao sema: Mola
wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika Akhera hana sehemu yoyote.
Maelezo

201.
Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera
mema, na utulinde na adhabu ya Moto!

Maelezo

202.
Hao ndio watakao pata sehemu yao kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

Maelezo

203.
Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa. Lakini mwenye
kufanya haraka katika siku mbili (akarejea) si dhambi juu yake; na mwenye
kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumchamngu. Na mcheni Mwenyezi
Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.
Maelezo

204.
Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia
hukufurahisha; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo moyoni mwake, na
hali yeye ndiye mkubwa wa ukhasimu.

Maelezo

205.
Na anapo tawala hufanya juhudi katika nchi kwa kufisidi humo na kuteketeza
mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.
Maelezo

206.
Na akiambiwa: Mwogope Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi.
Basi huyo inamtosha Jahannam. Paovu mno hapo kwa mapumziko.
Maelezo

207.
Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi
Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
Maelezo

208.
Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za
She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.
Maelezo

209.
Na ikiwa mkateleza baada ya kukufikieni hoja zilizo wazi, basi jueni kuwa
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Maelezo

210.
Je wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na
Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa? Na kwa Mwenyezi Mungu ndio hurejeshwa
mashauri yote.
Maelezo

211.
Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara ngapi zilizo wazi? Na anaye zibadili
neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali
wa kuadhibu.
Maelezo

212.
Walio kufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na wanawafanyia maskhara walio
amini. Na wenye kuchamngu watakuwa juu yao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu
humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

Maelezo

 
213.
Watu wote walikuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na
waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu
katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa
Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina
yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki
katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye
Njia Iliyo Nyooka.
Maelezo

214.
Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyo wajia wale walio
pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walio
amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Mwenyezi Mungu itakuja? Jueni kuwa
nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.

Maelezo

215.
Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayo itoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa
na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi
Mungu anaijua.
Maelezo

216.
Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachusha kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu
nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi
Mungu anajua na nyinyi hamjui.

Maelezo

217.
Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita
wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika Njia ya
Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti
Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka
wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini
yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani
na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.
Maelezo

218.
Hakika wale walio amini na wale walio hama na wakapigania Njia ya Mwenyezi
Mungu, hao ndio wanao taraji rehema za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.

Maelezo

219.
Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na
manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na
wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu
anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri--
Maelezo

220.--katika
mambo ya dunia na mambo ya Akhera. Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema:
Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na
Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angeli
penda angeli kutieni katika udhia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na
Mwenye hikima.
Maelezo

221.
Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora
kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume
washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko
mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Mwenyezi Mungu
anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake. Naye huzibainisha Aya zake
kwa watu ili wapate kukumbuka.

Maelezo

222.
Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake
wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wat'ahirike. Wakisha t'ahirika basi
waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda
wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha.
Maelezo

223.
Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini
jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika
nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini.
Maelezo

224.
Wala msifanye jina la Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa ni kisingizio cha
kuacha kufanya wema na kuchamngu na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
Maelezo

225.
Mwenyezi Mungu hakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi. Bali anakushikeni kwa
yanayo chuma nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
Maelezo

226.
Kwa wanao apa kuwa watajitenga na wake zao, wangojee miezi mine. Wakirejea basi
Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Maelezo

227.
Na wakiazimia kuwapa talaka basi, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mjuzi.
Maelezo

228.
Na wanawake walio achwa wangoje peke yao mpaka t'ahara (au hedhi) tatu zipite.
Wala haiwajuzii kuficha alicho umba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa
wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya
kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya sulhu. Nao wanawake wanayo
haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi
kuliko wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Maelezo

229.T'alaka
ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali
kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa
ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa
kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu hapo itakuwa hapana
lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi
msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhaalimu.
Maelezo

230.
Na kama amempa t'alaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hayo mpaka
aolewe na mume mwengine. Na akiachwa basi hapana ubaya kwao kurejeana wakiona
kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi
Mungu anayo ibainisha kwa watu wanao jua.
Maelezo

231.
Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi
warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru
mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake. Wala
msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni neema ya
Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima anacho
kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Maelezo

232.
Na mtakapo wapa wanawake t'alaka nao wakamaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa
na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule
miongoni mwenu anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni bora
zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, lakini nyinyi hamjui.
Maelezo

233.
Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kaamili kwa anaye taka
kutimiza kunyonyesha. Na juu ya baba yake chakula cha kina mama, na nguo zao
kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Mama
asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala baba kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya
mrithi mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa
kuridhiana na kushauriana, basi si vibaya kwao. Na mkitaka kuwapatia watoto
wenu mama wa kuwanyonyesha basi hapana ubaya kwenu mkitoa mlicho ahidi kwa
mujibu wa ada. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu
anayaona yote mnayo yatenda.

Maelezo

234.
Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake, hawa wake wangoje peke yao
miezi mine na siku kumi. Na wanapo timiza eda yao basi hapana ubaya kwao kwa
wanao jifanyia kwa mujibu wa ada. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo
yatenda.
Maelezo

235.
Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo
edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi
mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie
kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua
yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.

Maelezo

236.
Hapana ubaya kwenu mkiwapa t'alaka wanawake ambao hamjawagusa au kuwabainishia
mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kadiri awezavyo na
mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza kwa mujibu wa dasturi kuwa ni haki juu
ya watendao mema.
Maelezo

237.
Na mkiwapa t'alaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari
makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio agana, isipo kuwa ikiwa wanawake
wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi mwake awe
amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau
fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Maelezo

238.
Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi
Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).
Maelezo

239.
Ikiwa mnakhofu (Salini) na hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapo
kuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyo kufunzeni yale
mliyo kuwa hamyajui.
Maelezo

240.
Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakawacha wake, na wausie kwa ajili ya
wake zao kupata matumizi kwa mwaka mmoja bila ya kuwatoa nyumba. Na wanawake
wenyewe wakiondoka, basi hapana ubaya kwenu kwa waliyo jifanyia wenyewe kwa
mujibu wa Sharia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Maelezo

241.
Na wanawake walio achwa wapewe cha kuwaliwaza kwa mujibu wa Sharia. Haya ni
waajibu kwa wachamngu.
Maelezo

242.
Namna hivi anakubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake ili mpate kufahamu.
Maelezo

243.
Hukuwaona wale walio toka majumbani kwao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Mwenyezi
Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha akwahauisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.
Maelezo

244.
Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni
Msikizi na Mjuzi.
Maelezo

245.
Ni nani atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema ili amzidishie mzidisho
mwingi, na Mwenyezi Mungu hukunja na hukunjua. Na Kwake Yeye mtarejea.
Maelezo

246.
Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipo mwambia Nabii
wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je,
haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto
wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni
mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
Maelezo

247,
Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni
mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi
kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu
amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na
Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na
Mjuzi.
Maelezo

248.
Na Nabii wao akawaambia: Alama ya ufalme wake ni kukuleteeni lile sanduku
ambalo mna ndani yake kituliza nyoyo zenu, kitokacho kwa Mola wenu Mlezi, na
mna mabaki ya waliyo yaacha kina Musa na kina Harun, wanalichukua Malaika. Bila
shaka katika hayo zimo dalili kwenu ikiwa nyinyi mnaamini.
Maelezo

249.
Basi Taluti alipo ondoka na majeshi alisema: Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa
mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami:
ila atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo
kuwa wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja
naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye
yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi
makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye
kusubiri.
Maelezo

250,
Na walipo toka kupambana na Jaluti na majeshi yake walisema: Mola wetu Mlezi!
Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utusaidie tuwashinde watu
Makafiri--
Maelezo

251.--Kwa
idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi
Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa watu basi dunia ingeli haribika. Lakini
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote.
Maelezo

252.
Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na hakika wewe ni miongoni
mwa Mitume.
Maelezo

253.
MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao
Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana
wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia
hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na
wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli
pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.
Maelezo

254.
Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni kabla haijafika Siku ambayo
hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi. Na makafiri ndio madhaalimu.
Maelezo

255.
Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele.
Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na
duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua
yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio
katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na
duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye
Mkuu.
Maelezo

256.
Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu.
Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata
kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia,
Mwenye kujua.
Maelezo

257.
Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza
mwangazani. Lakini walio kufuru, walinzi wao ni Mashet'ani. Huwatoa kwenye
mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.
Maelezo

258.
Hukumwona yule aliye hojiana na Ibrahim juu ya Mola wake Mlezi kwa sababu
Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim alipo sema: Mola wangu ni yule ambaye
huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibrahim
akasema: Mwenyezi Mungu hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe
magharibi. Akafedheheka yule aliye kufuru; na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu.
Maelezo

259.
Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu tu, akasema:
Ataufufuaje Mwenyezi Mungu mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu
alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je umekaa muda
gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akamwambia: Bali
umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako,
havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni Ishara kwa
watu iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama.
Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu
ya kila kitu.
Maelezo

260.
Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu.
Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu
utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila
kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu
ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
Maelezo

261.
Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa
punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na
Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na
Mwenye kujua.
Maelezo

262.
Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishii masimbulizi
wala udhia kwa walicho toa, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa
khofu juu yao wala hawatahuzunika.

Maelezo

263.
Kauli njema na usamehevu ni bora kuliko sadaka inayo fuatiliwa na maudhi. Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha na Mpole.
Maelezo

264.
Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anaye
toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya
Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo,
kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote
kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Maelezo

265.
Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na
kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia
mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama haifikiwi na mvua kubwa
basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Maelezo

266.
Je! Yupo mmoja wenu anaye penda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo
mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia naye
hali ana watoto wanyonge, kikapigwa na kimbunga chenye moto, kikaungua? Hivi
ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Ishara ili mpate kufikiri.
Maelezo

267.
Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile
tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali
nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.
Maelezo

268.
Shet'ani anakutieni khofu ya ufakiri na anakuamrisheni mambo machafu. Na
Mwenyezi Mungu anakuahidini msamaha na fadhila zitokazo kwake. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.

Maelezo

269.
Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima bila ya shaka amepewa kheri
nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.
Maelezo

270.
Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo weka basi hakika Mwenyezi Mungu anajua.
Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.

Maelezo

271.
Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha mkawapa mafakiri kwa siri basi
hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi ya maovu yenu. Na Mwenyezi
Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.

Maelezo

272.
Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na kheri
yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu. Wala msitoe ila kwa kutafuta wajihi wa
Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mtakayo toa mtalipwa kwa ukamilifu, wala
hamtadhulumiwa.
Maelezo

273.
Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia za Mwenyezi Mungu, wasio weza
kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye wajua hali zao huwadhania kuwa ni
matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao;
hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa, basi kwa yakini
Mwenyezi Mungu anaijua.

Maelezo

274.
Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao
kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Maelezo

275.
Wale walao riba hawasimami ila kama anavyo simama aliye zugwa na Shet'ani kwa
kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi
Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliye fikiwa na
mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo
kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao
ndio watu wa Motoni, humo watadumu.

Maelezo

276.
Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu
hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi.
Maelezo

277.
Hakika wale walio amini na wakatenda mema na wakashika Sala na wakatoa Zaka,
wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala
hawatahuzunika.
Maelezo

278.
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa
nyinyi ni Waumini.
Maelezo

279.
Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu,
basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe.
Maelezo

280.
Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkiifanya
deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
Maelezo

281.
Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi
italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa.
Maelezo
282.
Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi andikeni. Na
mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika.
Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye deni juu yake aandikishe;
naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani
yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi
kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe
mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi
mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili
ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae
waitwapo. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake.
Hayo ndiyo haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa
ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya
mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini
mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na
mkifanya hivyo basi hakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu anakufundisheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Maelezo

283.
Na mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, yatosha kukabidhiwa rahani. Na mmoja
wenu akimwekea amana mwenziwe basi aliye aminiwa airudishe amana ya mwenzake,
na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala msifiche ushahidi. Na atakaye
ficha basi hakika moyo wake ni wenye kutenda dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
wa mnayo yatenda.
Maelezo

284.
Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya Mwenyezi Mungu. Na mkidhihirisha
yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu atakuhisabuni kwayo.
Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
uweza juu ya kila kitu.

Maelezo

285.
Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini
vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na
Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini)
husema: Tumesikia na tumet'ii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo
ni kwako.
Maelezo

286.
Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyho. Faida ya
iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu yake pia.
(Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu
Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola
wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na
uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya
makafiri.
Share on Google Plus

About DAIMA ANGAZA

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment