BIBLIA NA MTUME MOHAMED


Home
kabah
25 Swafar 1438 H

3) Ubashiri wa Kibiblia Juu ya Ujio wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mtume wa Uislamu

Ubashiri wa kibiblia juu ya ujio wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ushahidi wa ukweli wa Uislamu kwa watu wanaoiamini Biblia. Katika Kumbukumbu la Torati 18, Muusa alisema kuwa Mwenyezi Mungu alimwambia: “Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Hata itakuwa mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.” (Kumbukumbu la Torati 18:18-19) [40]
Kutokana na Aayah hizi, tunakhitimisha kwamba mtume aliyebashiriwa hapa lazima awe na sifa tatu zifuatazo:
  1. Kwamba atakuwa kama Muusa
  2. Kuwa atakuja kutoka kwa ndugu za Waisraeli, yaani uzawa wa Isma’iyl
  3. Mwenyezi Mungu atatia maneno yake kinywani mwa mtume huyo na akuwa atatangaza kile anachoamrishwa na Mwenyezi Mungu.
Hebu tuziangalie sifa hizi kwa undani zaidi.
1) Mtume Mfano wa Muusa
Hakukuwahi kutokea Mitume wawili wenye kufanana kama walivyokuwa Muusa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhim wa sallam). Wote wawili walipewa pana pamoja na mfumo wa taratibu na kanuni za maisha. Wawili hao walipambana na maadui wao na wakaibuka washindi kwa namna za kimiujiza. Wote wawili walikubalika kama Mitume na wakuu wa dola. Wote walitoroka baada ya njama za kutaka kuwaua. Kumfananisha Muusa na Yesu kumeacha kutilia maanani, si mfanano huo uliotajwa tu, bali pia nyingine zilizo muhimu sana. Hizo ni pamoja na kuzaliwa kwa njia ya kawaida, maisha yao ya kifamilia na kifo cha Muusa na cha Muhammad kufanana, lakini si cha Yesu. Zaidi ya hayo, Yesu alichukulika na wanafunzi wake kuwa Mwana wa Mungu wala si Mtume wa Mungu tu, tofauti na walivyokuwa Muusa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhim wa sallam), na kinyume kabisa na namna Waislamu wanavyoamini nafasi ya Yesu ilivyokuwa. Hivyo, ubashiri huu unamkusudia Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wala si Yesu, kwa sababu Muhammad anafanana zaidi na Muusa kuliko alivyo Yesu.
        Kadhalika, ukiangalia katika Injili ya Yohana, utakuta kuwa wayahudi walikuwa wakisubiri kukamilika kwa bishara tatu tofauti tofauti: 1) Kuja kwa Kristo, 2) Kuja kwa Eliyah, 3) Kuja kwa Mtume. Jambo hili liko wazi katika maswali matatu aliyoulizwa Yohana Mbatizaji:Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalem ili wamuulize, ‘Wewe u nani?’ Naye alikiri, wala hakukana, alikiri kwamba, ‘Mimi siye Kristo.’ Wakamwuliza, ‘Ni nini basi? U Eliya wewe?’ Akasema, ‘Mimi siye.’ ‘Wewe u nabii yule?’ Akajibu, ‘La.’” (Yohana 1:19-21)

Ikiwa tutaangalia ndani ya Biblia kwa marejeo mtambuko (ili kupata maelezo zaidi), tutakuta katika maelezo ya pembeni ambapo maneno “Mtume yule” yanapotokea katika Yohana 1:21 kwamba maneno haya yanakusudia ubashiri wa kwenye Kumbukumbu la Torati 18:15 na 18:1 [41]. Kutokana na hayo, tunakhitimisha kuwa Yesu si mtume yule aliyetajwa katika Kumbukumbu la Torati 18:18.

2) Kutoka kwa Ndugu za Waisraeli
Ibraahiym alikuwa na watoto wawili, Isma’iyl (Ishmaeli) na Is-haaq (Isaac). Isma’iyl akawa babu (asili ya) taifa la Waarabu na Is-haaq akawa babu wa taifa la Wayahudi. Mtume anayezungumziwa si wa kutokana na Wayahudi wenyewe, bali ni kutoka kwa miongoni mwa ndugu zao, yaani, uzao wa Isma’iyl. Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), atokanaye na uzawa wa Isma’iyl, ndiye khasa Mtume huyo.
Kadhalika, Isaya 42:1-13 inazungumzia kuhusu mtumishi wa Mungu, “mteule” Wake na “mtume” ambaye ataleta sheria duniani. “Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.” (Isaya 42:4). Aya ya 11 inamuunganisha mtume huyo mwenye kusubiriwa pamoja na uzao wa Kedar. Kedar ni nani? Kwa mujibu wa Mwanzo 25:13, Kedar alikuwa mtoto wa pili wa Isma’iyl (Ishmael), mmojawapo wa babu wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
3) Mwenyezi Mungu Atatia Maneno Yake Kinywani mwa Mtume Huyu
Maneno ya Mwenyezi Mungu (Qur-aan Tukufu) ni kweli yaliwekwa kinywani mwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mwenyezi Mungu Alimtuma Malaika Jibriyl kumfundisha Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) maneno khasa ya Mwenyezi Mungu (Qur-aan Tukufu) na akamuomba awasomee watu sawa na alivyoyasikia. Hivyo, maneno si yake yeye.
Hayakutokana na fikra zake mwenyewe, bali yalitiwa mdomoni mwake kupitia kwa Malaika Jibriyl. Katika wakati wa uhai wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na chini ya usimamizi wake, maneno haya yalihifadhiwa vichwani na yaliandikwa pia na Maswahaba wake.
Tambua kuwa Mwenyezi Mungu Alisema katika ubashiri wa kwenye Kumbukumbu la Torati: “Hata itakuwa mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.” (Kumbukumbu la Torati 18:19). Hii inamaanisha kuwa, yeyote mwenye kuiamini Biblia ni lazima aamini anachokisema mtume huyu, na mtume huyu ni Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
(Tafadhali tembelea www.islam-guide.com/mib kwa ajili ya maelezo zaidi juu ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Biblia.)



[40] Aya za Biblia katika kitabu hiki zimechukuliwa kutoka katika The Holy Bible in Kiswahili, Union Version, Published as Biblia, Maandiko Matakatifu, chapa ya mwaka 1997 ambayo ilichapishwa kwa ushirikiano wa Bible Society of  Tanzania na Bible Society of Kenya.
[41] Angalia maelezo ya pembeni katika The NIV Study Bible, New International Version katika aya ya 1:21 uk. 1594. Pia angalia katika The Holy Bible in Kiswahili, Union Version, Published as Biblia, Maandiko Matakatifu, chapa ya mwaka 1997 ambayo ilichapishwa kwa ushirikiano wa Bible Society of  Tanzania na Bible Society of Kenya, katika aya 1:21 uk. 92.
Share on Google Plus

About DAIMA ANGAZA

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment